CAPE TOWN-Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeendelea kung’ara kimataifa baada ya kushinda tuzo ya “Infrastructure Finance Deal of the Year 2026” zinazotolewa na Global Banking & Markets, kufuatia mafanikio ya upatikanaji wa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.78 kwa ajili kugharamia ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme (SGR) kwa kipande cha tatu na cha nne.
Tuzo hiyo imepokelewa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, kwa niaba ya Wizara ya Fedha katika hafla ya utoaji Tuzo za Global Banking & Markets iliyofanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini.Ushindi huo unatokana na mpango mahiri wa utafutaji ufadhili wa mradi huo mkubwa wa kimkakati, unaotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kurahisisha usafirishaji nchini na Ukanda wa Maziwa Makuu, mkopouliopatikana kupitia ushirikiano kati ya taasisi za bima kutoka nchi za Sweden, Poland na Italy pamoja na Benki za Maendeleo za Kikanda, chini ya uratibu wa Benki ya Standard Chartered.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wameilezea tuzo hiyo kuwa inatokana na maelekezo pamoja uongozi thabiti wa Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu usimamizi wa deni la Serikali pamoja na upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu.
“Tuzo hii ni ushindi unaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri kwenye masoko ya fedha ya kimataifa, ukiakisi uwezo wa nchi kubuni na kutekeleza mikataba mikubwa ya kifedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati ya maendeleo, pamoja na kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi,” alisema Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, Waziri wa Fedha wa Tanzania.
Tuzo za Global Banking & Markets, ambazo zimekuwa zikitolewa tangu mwaka 2014, hulenga kutambua nchi na taasisi zilizofanikiwa kuingia mikataba bora ya kifedha kupitia masoko ya mitaji na mikopo, huku vigezo vinavyozingatiwa ni pamoja na ubunifu wa muundo wa kifedha, unafuu wa masharti ya mikataba, pamoja na ubora wa utekelezaji wa mipango ya ufadhili wa miradi husika.
Tukio hili limekuja siku chache baada ya Tanzania kuibuka mshindi wa jumla wa mwaka katika Tuzo za Usimamizi wa Deni la Umma za Jumuiya ya Madola na pia kutwaa tuzo ya Ofisi Bora Kanda ya Afrika kupitia Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha (Debt Management Division), iliyotolewa jijini London, nchini Uingereza.
