PRETORIA-Kikao cha Kamati ya Fedha cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kinafanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini leo Machi 09, 2026 kujadili hali ya fedha ya jumuiya hiyo muhimu katika mtangamano wa kikanda kusini mwa Afrika.
Watalaamu wa masuala ya fedha na bajeti kutoka Tanzania, wakiongozwa na Kamishna wa Fedha za Nje katoka Wizara ya Fedha, Bw. Rishade Bade wanashiriki kikao hicho.
Miongoni mwa ajenda zinazojadiliwa ni pamoja na hali ya michango ya nchi wanachama wa SADC; mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya SADC ya mwaka 2025/26 kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia Aprili, 2025 hadi Desemba, 2025; mapendekezo ya bajeti mpya kwa mwaka wa fedha 2026/2027; na makadirio ya mapato na matumizi ya SADC kwa kipindi cha muda wa kati (2027/28-2030/31).
Ajenda nyingine zitakazojadiliwa kwa kina ni pamoja na vyanzo mbalimbali vya fedha (resources mobilization) kwa ajili ya kugharamia miradi ya kikanda na utekelezaji wa uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kanda (Regional Development Fund-RDF).Nchi 11 kati ya 16 za SADC ikiwemo Tanzania zimesaini mkataba wa uanzishwaji wa mfuko huo ambao utakuwa na jukumu la kugharamia miradi ya maendeleo katika kanda hiyo.
Kikao cha Kamati ya Fedha ni moja ya vikao vya utangulizi kuelekea Mkutano wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo utakaofanyika Machi 12 na 13. 2026.










