DAR-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amepokea rasmi nakala ya Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu leo Machi 3, 2026.

Mheshimiwa Kombo amempongeza Balozi Karemu kwa uteuzi wake na kueleza kuwa, wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ubalozi wa Kenya katika kipindi chake cha uwakilishi. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamejadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya, ikiwemo jitihada za kuondoa vikwazo vya kibiashara (NTBs) ili kurahisisha biashara kati ya raia wa nchi hizo jirani.
Aidha, wameangazia hatua za kuongeza thamani ya mazao ya biashara ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa manufaa ya uchumi wa kikanda.
Mazungumzo hayo pia yamegusia maandalizi yanayoendelea ya Kikao cha Wakuu wa Nchi wa EAC kinachotarajiwa kufanyika Machi 7, jijini Arusha.






