NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo ya kimkakati yanayolenga kuimarisha usalama wa nishati, kuongeza ufanisi wa bandari na kulinda mapato ya taifa.
Muonekano wa eneo la Mradi wa ujenzi wa Matenki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa Matenki hayo utasaidia kupunguza au kuondoa kabisa uhaba wa mafuta nchini, kuimarisha usalama wa nishati hiyo, kupunguza muda wa meli kusubiri nangani kutoka wastani wa siku 22 hadi siku 7, kupunguza muda wa kushusha shehena ya mafuta kutoka siku 7 hadi siku 1, kuongeza mapato ya Taifa kupitia makusanyo ya kodi na tozo mbalimbali zitakazokusanywa na mamlaka husika pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.
Maagizo hayo ameyatoa Machi 3,2026 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa matenki ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt.Samia ameitaka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati, kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya ubora na usalama.
Pia, amesisitiza kuwa,utekelezaji madhubuti wa mradi huo ni nyenzo muhimu katika kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu imara cha biashara ya nishati katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Aidha, Rais ameielekeza Wizara ya Nishati kuimarisha akiba ya kimkakati ya mafuta ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na mabadiliko ya bei katika soko la dunia.
Amebainisha kuwa,mazingira ya sasa ya uchumi wa kimataifa yanahitaji nchi kuwa na hifadhi thabiti ya nishati ili kulinda uchumi wake dhidi ya mitikisiko ya nje.
Katika kulinda mapato ya umma, Rais Dkt. Samia ameiagiza TPA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na taasisi nyingine za serikali kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa vipimo na shehena za mafuta kuanzia hatua ya upakuaji bandarini hadi usambazaji wake.
Amesisitiza umuhimu wa mifumo ya kidijitali kusomana ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya taifa na kuongeza uwazi katika mnyororo mzima wa thamani wa mafuta.
Rais Dkt.Samia amesema, suala la mifumo kusomana ni muhimu ili kusiwe na mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.
Vilevile, ameeleza kuwa, maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya uchukuzi yameleta mageuzi chanya katika utendaji wa bandari nchini, hatua inayoiwezesha Tanzania kupokea na kuhudumia meli kubwa zinazofanya safari katika bandari kuu za kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo ya Mradi wa ujenzi wa Matanki ya kupokea Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Kigamboni jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Machi, 2026. Ujenzi wa matenki hayo utasaidia kupunguza uhaba wa mafuta nchini, kupunguza muda wa meli kusubiri nangani kutoka wastani wa siku 22 hadi siku 7, kupunguza muda wa kushusha shehena ya mafuta kutoka siku 7 hadi siku 1, kuongeza mapato ya Taifa pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi Mradi wa ujenzi wa Matenki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Machi, 2026.
Ameongeza kuwa, uwekezaji huo umeongeza ufanisi wa huduma za upakuaji na upokeaji mizigo, na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.Kwa mujibu wa Rais, mafanikio hayo yamechangia kuongezeka kwa mapato ya serikali kupitia kodi ya forodha na kufikia zaidi ya Shilingi trilioni 12, jambo linaloongeza uwezo wa serikali kugharamia miradi ya maendeleo na kuimarisha uchumi wa taifa.
Amebainisha pia kuwa,ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari ni mkakati mahsusi wa kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji kwa TPA, huku mamlaka hiyo ikielekeza rasilimali zaidi katika uwekezaji wa miundombinu mipya na ya kisasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema, kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa kinara wa huduma za upakuaji na uhifadhi wa mafuta katika ukanda huo.
Ameeleza kuwa,wizara yake imejikita katika kuimarisha mnyororo wa usafirishaji na usambazaji wa mizigo, hatua iliyosaidia kupunguza msongamano uliokuwa ukiikumba Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Miongoni mwa matokeo chanya yaliyopatikana ni kuongezeka kwa kasi ya upakuaji na upakiaji mizigo, kupungua kwa muda wa meli kukaa bandarini, pamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuweka jiwe la msingi Mradi wa Ujenzi wa Matenki ya kupokea Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Kigamboni jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Machi, 2026.Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa amesema kuwa, hadi Machi 2, 2026, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 41, na kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika Februari,2027.
Amefafanua kuwa,kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa upakuaji wa mafuta kutoka wastani wa siku 22 hadi siku saba, hatua itakayopunguza msongamano wa meli bandarini na kuongeza ushindani wa bandari hiyo kimataifa.
Mbossa amesema, mradi utaondoa changamoto ya uhamishaji wa mafuta kwa njia ya mileti kutoka kwenye gati na kupunguza tozo ya ucheleweshaji wa upakuaji, ambayo kwa sasa hufikia wastani wa Shilingi milioni 28 kwa kila meli kwa siku.
Kwa ujumla, utekelezaji wa mradi huo unaonekana kuwa kichocheo muhimu cha mageuzi ya sekta ya nishati na uchukuzi nchini, ukiiweka Tanzania katika nafasi bora ya ushindani wa kikanda na kimataifa, sambamba na utekelezaji wa mipango ya maendeleo kuelekea Dira ya Taifa ya 2050.
Tags
Bandari ya Dar es Salaam
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Matenki ya Mafuta Bandarini
TPA Tanzania







