Waziri wa Fedha aipongeza YAS Tanzania kwa kukuza Sekta ya Mawasiliano nchini

DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ameipongeza,Kampuni ya Mawasiliano ya YAS Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya mawasiliano nchini na kuitaka iongeze uwekezaji katika miundombinu na huduma za mawasiliano ya kidijitali ili kuendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Mhe. Omar ametoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Kampuni ya YAS Tanzania katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili masuala ya uwekezaji na nafasi ya sekta ya mawasiliano katika kuharakisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya teknolojia nchini.

Amesema,YAS Tanzania ni miongoni mwa kampuni kubwa za mawasiliano nchini ambazo zimeendelea kuwa washirika muhimu wa Serikali katika kuendeleza huduma za mawasiliano na teknolojia ya habari.
"Licha ya mabadiliko ya umiliki na majina ya kampuni ya YAS Tanzania kwa nyakati tofauti, mchango wake katika sekta ya mawasiliano umeendelea kuonekana tangu ilipoanza shughuli zake kama Mobitel katika hatua za awali za huduma za mawasiliano ya simu nchini."

Mhe. Balozi Omar, aliipongeza YAS Tanzania kwa kuwekeza takribani shilingi trilioni 1.4 katika kipindi cha miaka minne iliyopita, katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini, hatua ambayo imechangia kupanua huduma za mawasiliano na kukuza uchumi wa kidijitali.

Aidha, aliongeza kuwa, Kampuni hiyo imelipa kodi ya takribani shilingi bilioni 576 katika kipindi cha miaka minne, mchango unaosaidia kuongeza mapato ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Mbali na uwekezaji na ulipaji wa kodi, naipongeza YAS kwa kushiriki katika maendeleo ya jamii kupitia miradi ya kijamii, ulinzi wa mazingira pamoja na kuwajengea vijana uwezo katika ujuzi wa kidijitali na teknolojia, hatua ambayo ni muhimu katika kuandaa nguvu kazi ya Taifa kwa uchumi wa kisasa,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Mhe. Balozi Omar aliisihi YAS Tanzania kuendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya mawasiliano, akisisitiza kuwa sekta hiyo ina nafasi kubwa ya kuchangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau wa sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha sekta hiyo inatoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya YAS Tanzania, Bw. Pierre Canton Bacara, alisema kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini, kwa kuwekeza katika teknolojia za kisasa, kupanua huduma za mawasiliano na kuchangia katika juhudi za Serikali za kuharakisha mageuzi ya kidijitali yanayolenga kuongeza tija ya uchumi na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.

Bw. Bacara aliongeza kuwa, kupitia uwekezaji huo, YAS imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na fedha kidijitali kwa Watanzania wengi zaidi, sambamba na kuunga mkono malengo ya Serikali ya kujenga uchumi shirikishi unaotegemea teknolojia na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kupanua huduma za kidijitali, kuongeza ubunifu na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.
"Nikuhakikishie lengo letu ni kuwa mshirika wa kuaminika wa kidijitali kwa Serikali ya Tanzania katika kusaidia utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya muda mrefu ya nchi, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mfumo wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali (2024–2034) kwa kuwa Miundombinu ya kidijitali iliyo imara na jumuishi ni msingi muhimu wa kuongeza tija ya uchumi na ubunifu, kukuza ujumuishaji wa kifedha na ukuaji wa biashara ndogo na za kati (SMEs), pamoja na kupanua huduma za serikali mtandaoni na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato,” alisema Bw. Bacara

Alieleza kuwa, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kampuni hiyo imewekeza zaidi katika upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya mtandao, huku mtandao wake wa 4G na 5G ukiwafikia zaidi ya asilimia 95 ya Watanzania, na zaidi ya wateja milioni 22 wanatumia huduma za kifedha za Mixx, wakifanya miamala inayozidi shilingi trilioni 7, huku zaidi ya mawakala 250,000 na wafanyabiashara zaidi ya 500,000 wakitumia mfumo wa malipo wa Lipa Kwa Simu unaochakata zaidi ya shilingi bilioni 700 kila mwezi, hatua inayochochea ujumuishaji wa kifedha na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here