Waziri wa Fedha apongeza ushirikiano uliopo kati ya Serikali,sekta ya fedha na sekta binafsi katika kujenga uchumi imara wa Taifa

DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesifu ushirikiano uliopo kati ya Serikali, sekta ya fedha na sekta binafsi katika kujenga uchumi imara wa Taifa.
Mhe. Balozi Omar, ametoa pongezi hizo wakati akihutubia katika tukio la futari maalum iliyoandaliwa na Benki ya NBC kwa ajili ya wateja wake, katika Hoteli ya Rotana, Jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweka msisitizo mkubwa katika kujenga uchumi jumuishi, shindani na unaotegemea uzalishaji ambao mafanikio yake yanahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Alisema kuwa Sekta ya fedha ina nafasi ya msingi katika maendeleo ya nchi na kwamba uchumi hauwezi kukua bila mfumo wa fedha ulio thabiti, unaoaminika na unaowafikia wananchi. wawekezaji na wafanyabiashara kwa wakati.
“Nyote mnafahamu malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ya kujenga Tanzania yenye uchumi wa kisasa unaochochewa na uwekezaji, viwanda, biashara na ubunifu wa kidijitali. Ili kufikia malengo hayo, sekta ya fedha na hasa benki zina jukumu la msingi-si kama watoa huduma pekee, bali kama wawezeshaji wa mageuzi makubwa ya kiuchumi,”alisema Mhe. Balozi Omar.

Mhe. Balozi Omar aliwahakikishia wadau wa maendeleo kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira ya kuwezesha mchango wa benki katika uchumi uendane na matarajio ya Dira hiyo ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 Ili kukuza kwa haraka uchumi, ajira, kipato na ustawi kama jamii na Taifa.

Aidha, aliipongeza Benki ya NBC kwa kuendeleza utamaduni wa kuwakutanisha wateja wake na kuwaandalia futari hatua inayo imarisha mshikamano kati ya NBC na wateja wake.

Mwezi mtukufu wa Ramadhan unatukumbusha maadili ya imani, nidhamu, subira, uaminifu na uwajibikaji unatufundisha kujali utukufu wa muumba wetu, huruma na kujali,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Alisema kuwa hayo si maadili ya ibada pekee, bali ni msingi muhimu hata katika uendeshaji wa taasisi kwa kwa makundi yasiyo na hali nzuri ya kipato na kutoa kwa makundi mengine ya watu wenye uhitaji.

“Ndiyo maana tunathamini jitihada za taasisi za fedha zinazojenga ukaribu na wateja wao, kwa sababu uaminifu ndiyo msingi wa mzunguko wa fedha katika uchumi na ndiyo maana Ninaipongeza Benki ya NBC kwa kuendeleza utamaduni wa kukutana na kuwa karibu na wateja wake katika mazingira kama haya,” alisisitiza Mhe. Balozi Omar.

Kwa upande wao, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw. Theobald Sabi, na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Hiyo, Dkt. Elirehema Doriye waliipongeza Serikali kwa kuweka na kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini hatua iliyochangia kuimarika kwa biashara yao na kufanikisha upatikanaji wa mitaji kupitia mikopo kwa wateja wao.
Waliahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 iyotaka uchumi wa Taifa ufike dola za Marekani trilioni 1 ifikapo Mwaka 2050, iweze kufikiwa kupitia mchango wa Sekta ya umma na Sekta Binafsi.

Hafla hiyo ya futari iliwakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na wageni mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano, mshikamano na kuendeleza umoja wa kitaifa katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here