NA DIRAMAKINI
ALIYEKUWA Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Qutesh wilayani Hanang’ mkoani Manyara, Bw.Senesa Gidang’adi Machakwa amefikishwa mahakamani kwa makosa ya rushwa.

Machakwa amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hanang’ Aprili 13, 2026 na kufunguliwa shauri la Uhujumu Uchumi namba 7732/2026 mbele ya Mheshimiwa Ponella Iloni, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Hanang’.
Mshtakiwa anashtakiwa kwa kosa la ufujaji na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka akiwa mtumishi wa umma kinyume na kifungu cha 28(1) na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 R:E 2023.
Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Wilaya ya Hanang’,Bw. Daudi Kingazi ameieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitumia madaraka yake vibaya na kufanya ubadhirifu wa shilingi 800,000 kwa ajili ya ukodishaji wa mashamba ya kijiji na hakuwahi kuzifikisha katika akaunti ya kijiji hicho kinyume na kifungu cha 50(5) cha Memoranda ya Fedha za Serikali za Mitaa ya 2009.
Mshtakiwa amesomewa hati ya mashtaka na amekana kutenda kosa hilo. Mshtakiwa ametimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja, barua ya utambulisho ya serikali za mitaa pamoja na kusaini bondi ya shilingi 2,000,000 na kwa sasa yupo nje kwa dhamana.
Aidha,shauri hilo limehairishwa hadi Mei 5,2026 kwa ajili ya kusomwa hoja za awali.
Tags
Habari
Mahakamani Leo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Uhujumu Uchumi
Wilaya ya Hanang