Aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Endasaboghechan wilayani Hanang' mahakamani kwa tuhuma za kughushi nyaraka

MANYARA-Mahakama ya Wilaya ya Hanang’ Aprili 20, 2026 imefungua shauri la jinai namba 8355/2026 dhidi ya aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Endasaboghechan, Bw. Juma Raphael Iddi, anayekabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka za kifedha.
Shauri hilo limesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mheshimiwa Arnold Kileo, ambapo upande wa mashtaka ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wilaya ya Hanang’, Bw. Daudi Kingazi umeeleza kuwa, mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa hayo katika nyakati tofauti mwaka 2023.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Bw. Iddi anatuhumiwa kughushi saini za watia saini wa shule hiyo katika nyaraka mbalimbali za malipo pamoja na hundi, hatua iliyomwezesha kutoa fedha benki kinyume cha sheria.

Mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(d)(i) na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.

Baada ya kusomewa hati ya mashtaka, mshtakiwa alikanusha tuhuma zote zinazomkabili.

Mahakama imemruhusu mshtakiwa kuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa, pamoja na kusaini hati ya dhamana ya shilingi milioni mbili kwa kila mdhamini.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Mei 5, 2026, litakaporejeshwa mahakamani kwa ajili ya hatua ya usomaji wa hoja za awali (PH).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here