Watumishi sita wa Halmashauri ya Manyoni mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na wizi

SINGIDA-Watumishi sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Manyoni wakikabiliwa na mashitaka kadhaa ya jinai ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, wizi kwa mtumishi wa umma pamoja na kuisababishia mamlaka hasara.
Kesi hiyo ya Jinai Na. 8219/2026 ilifunguliwa rasmi Aprili 16, 2026, ikiwahusisha Bi. Devota Jonathan, mwalimu wa Shule ya Sekondari MesoMapya, pamoja na maafisa ugavi watano ambao ni Bw. Joseph Nswila, Bw. Charles Mpenzu, Bw. Oscar Silaa, Bw. Dennis Mbuma na Bw. Shabani Samu.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume na Kifungu cha 96(1) na (2) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya mwaka 2022) kinachohusu matumizi mabaya ya ofisi.

Aidha, wanakabiliwa na shtaka la wizi kwa mtumishi wa umma kinyume na Vifungu vya 265 na 270 vya sheria hiyo, pamoja na kosa la kuisababishia mamlaka hasara kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza, zikisomwa pamoja na Vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (Marejeo ya mwaka 2022).

Inadaiwa kuwa,katika kipindi cha kuanzia Mei 1, 2022 hadi Disemba 30, 2023, washtakiwa hao, wakiwa katika nyadhifa zao kama watunza stoo, walishindwa kurekodi ipasavyo kwenye daftari la ghala (store ledger) pamoja na hati za kutolea bidhaa (issue vouchers) jumla ya maboksi 308 ya vigae vyenye ukubwa wa milimita 240 kwa 400.

Vigae hivyo vinakadiriwa kuwa na thamani ya Shilingi 6,468,000, ambapo kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi kumesababisha upotevu wa mali hiyo ya umma.

Shauri hilo lilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, Mhe. George Kapama, ambapo upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Marshal Mseja.

Washtakiwa wote walikana mashitaka yanayowakabili na kwa sasa wapo nje kwa dhamana wakisubiri hatua zaidi za kisheria.

Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Aprili 29, 2026, ambapo itatajwa kwa ajili ya hoja za awali kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa ushahidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here