NA DIRAMAKINI
BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Kondoa, Bernardin Francis Mfumbusa kilichotokea Aprili 14,2026 majira ya saa 11:45 asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu ya dharura.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, marehemu Askofu Mfumbusa anatarajiwa kuzikwa Aprili 22,2026 katika Jimbo Katoliki la Kondoa, ambako alilitumikia kanisa kwa uaminifu mkubwa kama Askofu wa kwanza tangu kuanzishwa kwake.
Kifo chake kinakuja siku chache baada ya kuteuliwa kwake na Papa Leo XIV tarehe 9 Aprili 2026 kuwa Mjumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii.
Kabla ya uteuzi huo, Askofu Mfumbusa alikuwa Rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar (CEPACS), nafasi iliyodhihirisha umahiri wake mkubwa katika taaluma ya mawasiliano ya jamii ndani na nje ya bara la Afrika.
Kanisa Katoliki limempoteza mchungaji mwenye weledi wa hali ya juu na mtaalamu mbobezi wa mawasiliano ya jamii, aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha mawasiliano ya Injili kwa nyakati za kisasa.
Hayati Askofu Mfumbusa alizaliwa Aprili 1,1962 mjini Kondoa na amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 64.
Aidha, baada ya malezi na majiundo ya kikasisi, alipokea Daraja Takatifu la Upadre tarehe 14 Juni 1992 kutoka kwa Matthias Joseph Isuja, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma wakati huo.
Hatua muhimu katika huduma yake ilifikiwa Machi 11,2011, pale Papa Benedikto XVI alipounda Jimbo Katoliki la Kondoa na kumteua kuwa Askofu wake wa kwanza.
Aliwekwa wakfu rasmi Mei 15,2011 na Polycarp Pengo, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, akisaidiana na Yuda Thaddeus Ruwa'ichi na Augustine Ndeliakyama Shao.
Katika kipindi cha maisha yake ya utumishi, marehemu Askofu Mfumbusa alilihudumia Kanisa kama Padre kwa miaka 33 na baadaye kama Askofu kwa miaka 14, akitekeleza kwa uadilifu dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza waamini.
Kifo chake kinaacha pengo kubwa si tu kwa Jimbo la Kondoa bali pia kwa Kanisa Katoliki Tanzania na Afrika kwa ujumla, hasa katika nyanja ya mawasiliano ya jamii ambapo alikuwa mmoja wa vinara wake.
