BoT yawanoa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar

ZANZIBAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha semina maalum ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uelewa na utekelezaji wa kanuni mpya za huduma ndogo za fedha.
Semina hiyo ilifanyika katika Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu Zanzibar na kufunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dkt. Hamad Omar Bakari.

Akizungumza katika semina hiyo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anayesimamia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda K. Msemo, alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uelewa wa Wajumbe wa Kamati kuhusu sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wake.
Alieleza kuwa kanuni zilizowasilishwa zinajumuisha Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha Zanzibar (Watoa Huduma Wasiopokea Amana), 2025; Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha Zanzibar (Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo-SACCOS), 2025; pamoja na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha Zanzibar (Vikundi vya Kijamii), 2025.

Bi. Msemo alibainisha kuwa utekelezaji wa kanuni hizo utaongozwa na mikakati mbalimbali, ikiwemo kufanya vikao vya pamoja na Wizara ya Fedha, Idara ya Ushirika na Tawala za Mikoa ili kubaini idadi na mgawanyo wa kijiografia wa watoa huduma ndogo za fedha.

Katika hatua nyingine, Benki Kuu imejipanga kutoa elimu na mafunzo kwa watoa huduma ndogo za fedha kuhusu taratibu za kupata leseni na usajili kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Mafunzo hayo pia yatahusisha maafisa wa Idara ya Maendeleo ya Ushirika pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa watakaohusika na usimamizi wa taasisi za daraja la tatu na la nne.

Sambamba na hilo, BoT itaandaa miongozo ya usimamizi kwa watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja yote, pamoja na kuanzisha mifumo ya kielektroniki itakayowezesha usajili, upokeaji na uchakataji wa taarifa za kiutendaji kwa taasisi husika.
Washiriki wa semina hiyo walijumuisha Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati, viongozi kutoka Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar na Benki Kuu ya Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here