Magazeti leo Julai 20,2026

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga amemtembelea mwanatasnia mkongwe wa filamu na michezo ya kuigiza nchini, Fatuma Makongoro maarufu kama Bibi Mwenda nyumbani kwake Kivule, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuendelea kumjulia hali ya afya yake.
Bi Mwenda amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya magoti tangu mwaka 2015, hali iliyomlazimu kufanyiwa upasuaji wa magoti yote mawili.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa jitihada za TFB kuwafariji na kuwathamini wanatasnia waliochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya filamu na sanaa ya uigizaji nchini.

Ikumbukwe kuwa Dk Kasiga alimtembelea Bi Mwenda kwa mara ya kwanza Januari 17 mwaka huu kufuatia upasuaji wa goti la mguu wa kulia.

Kwa sasa, afya yake inaendelea kuimarika baada ya kukamilisha upasuaji wa magoti yote mawili, huku akiendelea na mazoezi ya tiba (physiotherapy) yanayomsaidia kurejesha nguvu na uwezo wa kutembea.




















Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenda alimshukuru Dk Kasiga pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania kwa upendo, faraja na ufuatiliaji wa karibu waliouonyesha tangu alipougua.

Ameeleza kuwa kuendelea kutembelewa na kutiwa moyo kumempa nguvu na matumaini katika safari yake ya matibabu, huku akiahidi kuendelea kupambana hadi atakapopona kabisa.

Kwa upande wake, Dk Kasiga alimtakia Bi. Mwenda afya njema na uponyaji wa haraka ili aweze kurejea katika shughuli zake akiwa na afya iliyoimarika zaidi.

Ameeleza kuwa uzoefu na mchango wake katika sekta ya filamu ni hazina muhimu kwa taifa, hususan katika kuendelea kulea na kuhamasisha kizazi kipya cha wanatasnia kuzingatia maadili, weledi na ubora katika kazi za filamu.

Katika ziara hiyo, Dk Kasiga aliambatana na waigizaji wakongwe nchini, Haji Salim (Mboto) pamoja na Said Mohamed (Boka) ambao kwa pamoja waliwahi kuwa sehemu ya Kundi la Kaole Sanaa.

TFB imeahidi kuendelea kuwakumbuka, kuwathamini na kuwaenzi wanatasnia wakongwe kama Bi Mwenda kwa mchango wao mkubwa katika kujenga na kukuza sekta ya filamu na michezo ya kuigiza nchini, kuibua vipaji vya wasanii wapya na kurithisha maarifa, uzoefu na misingi ya taaluma ya filamu kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here