Gavana wa BoT ashiriki mikutano ya IMF na Benki ya Dunia jijini Washington D.C

WASHINGTON D.C-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, pamoja na Naibu Gavana anayesimamia Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, wameshiriki katika Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB) iliyofanyika jijini Washington, D.C., Marekani kuanzia tarehe 13 hadi 18 Aprili 2026.
Mikutano hiyo hutoa fursa kwa viongozi wa uchumi na fedha duniani kujadili mwenendo wa uchumi wa dunia, kubaini changamoto zinazoikabili, na kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza uchumi jumuishi na endelevu. 

Pia, hutumika kama jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha.
Katika mikutano hiyo, masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo hali ya uchumi wa dunia, utulivu wa sekta ya fedha, usimamizi wa deni la umma, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na mchango wa teknolojia za kidijitali katika kuendeleza sekta ya fedha. 

Washiriki walisisitiza umuhimu wa kuimarisha biashara na ushirikiano wa kimataifa ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Pembezoni mwa mikutano hiyo, Gavana alishiriki katika kikao cha nchi za Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika la IMF, ambapo walipitia taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kundi hilo kwa mwaka 2026 na kujadili changamoto za sekta ya nje zinazoathiri uchumi wa nchi za Afrika, hususan athari za migogoro ya kimataifa.

Aidha, Gavana alifanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa maendeleo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, yakilenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kifedha.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na uendelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa.

Katika hatua nyingine, Gavana alikutana na taasisi za kifedha za kimataifa kwa lengo la kupanua wigo wa ushirikiano, hususan katika huduma za malipo ya kimataifa na ubadilishaji fedha, ili kuimarisha ufanisi wa mifumo ya kifedha nchini.

Vilevile, alishiriki katika mjadala maalum uliojadili namna ubunifu na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi unavyoweza kuchochea maendeleo ya biashara ndogo na za kati pamoja na biashara zinazoongozwa na wanawake.
Katika mjadala huo, Gavana alisisitiza dhamira ya BoT katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha, na kuharakisha matumizi ya teknolojia za kidijitali. Mjadala huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Alliance for Financial Inclusion (AFI) na Growth Firms Alliance (GFA).

Ushiriki wa Tanzania katika mikutano hiyo unaendelea kuwa kichocheo muhimu cha kupata maarifa, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, na kusaidia jitihada za kukuza uchumi wa taifa kwa manufaa ya wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here