TANGA-Wilaya ya Pangani mkoani Tanga imepiga hatua muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi wake kupitia utambulisho wa mradi wa uuzaji na usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku. Mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia, hususan kwa kaya zenye kipato cha chini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutambulisha mradi huo mbele ya katibu tawala wa Wilaya ya Pangani, Bi. Ester Gama, msimamizi wa mradi kutoka REA, Ndugu Abdulrazack Mkomi ameeleza kuwa lengo kuu la mradi huo ni kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, ambayo yamekuwa yakichangia uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kiafya kwa wananchi, hasa wanawake na watoto.
Alifafanua kuwa kupitia mradi huo, mitungi ya gesi ya kilo sita itapatikana kwa bei nafuu ya shilingi 17,500 tu kutokana na ruzuku iliyotolewa, hali itakayowezesha wananchi wengi zaidi kuimudu na kuanza kutumia nishati mbadala iliyo rafiki kwa mazingira.
Aidha, mfumo mzuri wa usambazaji umeandaliwa ili kuhakikisha mitungi hiyo inawafikia walengwa ambao ni wananchi waishio maeneo ya vijijini na mwananchi atatakiwa kuwa na kitambulisho cha taifa (NIDA) na pesa taslimu 17,500 ili kupata mtungi huo.
Kwa upande wake, Katibu tawala wa Wilaya ya Pangani aliupokea mradi huo kwa furaha na kupongeza juhudi za Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan , REA na wadau wengine waliowezesha utekelezaji wake.
Alisisitiza kuwa mradi huo ni hatua muhimu katika kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira, na kupunguza gharama za maisha kwa kaya nyingi.
“Mradi huu ni wa kimkakati kwa ustawi wa wananchi wetu. Tunatarajia kuona mabadiliko chanya katika matumizi ya nishati, na hivyo kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa,” alisema Katibu tawala.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo walieleza matumaini yao kuwa upatikanaji wa mitungi hiyo kwa bei ya ruzuku utarahisisha maisha yao ya kila siku, hasa katika shughuli za kupika. Wengi wao walionyesha utayari wa kuanza kutumia gesi badala ya njia za jadi.
Mradi huu unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya nishati ya kupikia katika Wilaya ya Pangani, huku ukichochea maendeleo endelevu na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa ujumla.









