NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Saudi Arabia imetangaza hatua kali za kudhibiti mahujaji kwa kupiga marufuku kabisa matumizi ya visa za ziara (visit visas) kushiriki ibada ya Hija, huku ikiweka masharti mapya ya kuingia katika miji mitakatifu ya Makka na Madina.
Picha kwa hisani ya AlharamainSA.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, kuanzia msimu wa Hija wa mwaka 2026, ni wale tu wenye vibali maalum vya Hija watakaoruhusiwa kuingia Makka na kushiriki ibada hiyo.
Hatua hiyo inalenga kudhibiti idadi ya mahujaji na kuhakikisha usalama pamoja na uratibu bora wa ibada hiyo kubwa duniani ya Kiislamu.
Mamlaka za Saudi Arabia zimeeleza kuwa, watu wote wanaotumia visa za muda mfupi, ikiwemo visa za utalii au ziara, hawataruhusiwa kabisa kuingia Makka wakati wa msimu wa Hija bila kibali rasmi.
Aidha, wale watakaokiuka masharti hayo watakumbwa na adhabu kali za kisheria.
Hatua hii pia inaambatana na kusimamishwa kwa utoaji wa vibali vya Umrah kwa muda maalum ili kutoa nafasi kwa maandalizi ya Hija na kupunguza msongamano wa waumini katika maeneo matakatifu.
Serikali imeonya kuwa,mtu yeyote atakayejihusisha na Hija bila kibali rasmi atatozwa faini inayoweza kufikia riyal 20,000 za Saudi Arabia, pamoja na uwezekano wa kufukuzwa nchini na hata kupigwa marufuku kurejea kwa muda mrefu.
Pia, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaosaidia au kuwezesha watu kuingia kinyume cha sheria katika maeneo ya Hija, ikiwa ni pamoja na wasafirishaji na mawakala wa safari.
Mamlaka zimeeleza kuwa,uamuzi huo ni sehemu ya mikakati ya kuboresha usimamizi wa Hija, ambayo hukusanya mamilioni ya Waislamu kutoka duniani kote kila mwaka.
Udhibiti huu unalenga kupunguza msongamano, kuimarisha usalama na kuhakikisha ibada inafanyika kwa utaratibu na utulivu zaidi.
Kwa ujumla, hatua hizi zinaashiria msisitizo mpya wa Saudi Arabia katika kuhakikisha kuwa ibada ya Hija inafanyika chini ya mfumo rasmi unaotambuliwa, huku ikiwataka waumini kufuata taratibu zote za kisheria kabla ya kupanga safari yao ya kidini.(gn)
