NA LWAGA MWAMBANDE
UKIREJEA katika neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu utaona kuwa, alfajiri ya siku ya tatu baada ya kusulubiwa simulizi inayotikisa historia ya mwanadamu inaanza upya ambapo kaburi lililokuwa limefungwa linakutwa wazi, na tumaini linaloonekana kufa linafufuka kwa nguvu isiyozuilika.
Hapo ndipo msingi wa imani ya Ukristo unapopata uthibitisho wake mkuu kupitia kufufuka kwa Yesu Kristo.
Kufufuka kwa Yesu Kristo na maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka ni kiini cha imani ya Kikristo, yakibeba maana ya kina ya kiroho, kijamii na kimaadili kwa waumini duniani kote.
Kwanza, tukio la kufufuka linatazamwa kama ushindi wa uhai dhidi ya kifo. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kikristo, Yesu alisulubiwa, akafa, na akazikwa, lakini siku ya tatu akafufuka.
Tukio hili linachukuliwa kuwa uthibitisho wa uungu wake na utimilifu wa ahadi za Mungu kwa wanadamu. Hivyo basi, kwa Wakristo, kufufuka si simulizi ya kihistoria tu bali ni msingi wa tumaini la uzima wa milele.
Pili, Pasaka huadhimisha ushindi huo wa Yesu dhidi ya dhambi na mauti. Ni kipindi cha furaha na shukrani kinachofuatia maombolezo ya mateso na kifo chake.
Katika muktadha huu, Pasaka huwahamasisha waumini kutafakari upya maisha yao, kuacha dhambi, na kuanza maisha mapya yaliyojaa haki na upendo.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, kwa Wakristo, kufufuka kwa Yesu ni ishara ya ushindi wa uhai dhidi ya kifo na uthibitisho wa ahadi ya uzima wa milele.
Aidha, maadhimisho ya Pasaka hubeba ujumbe wa matumaini, msamaha na mwanzo mpya, yakiwahamasisha waumini kuishi maisha ya haki, upendo na mshikamano katika jamii. Endelea;
1. Bwana Yesu kafufuka, hizi habari za kweli,
Watu wale walitoka, kuisema hii kweli,
Ni wale waaminika, kwa watu wao halali,
Kweli hainunuliki, kafufuka kweli kweli.
2. Mariamu Magdalena, yeye alipashwa kweli,
Kwamba kafufuka Bwana, alipolala mahali,
Hayupo akapaona, huo ujumbe halali,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
3. Kajibeba Mariamu, kwenda kutangaza kweli,
Si kwa wote wanadamu, kwa wanafunzi kamili,
Wale ndani walidumu, wanachunga zao hali,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
4. Wale aliwaambia, waliamini ni kweli,
Vema walimsikia, wakatulizana hali,
Ndivyo ilivyotukia, ilivyosambaa kweli,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
5. Na watesi wake Yesu, walotenda ujahili,
Kufufuka liwahusu, nao walipata kweli,
Ni yote si nusunusu, toka watu wao kweli,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
6. Wale wale maaskari, katika lindo halali,
Waliwapasha habari, Yesu amefufuka kweli,
Kwa makuhani ni shari, kusikia jambo hili,
Kafufuka kwelikweli, shangilia Haleluya.
7. Wakajaribujaribu, kufunika hiyo kweli,
Kwa rushwa kuiharibu, isisikike mahali,’
Waliyopata majibu, hainunuliki kweli,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
8. Hata ujaribu vipi, inajitetea kweli,
Hata uifiche vipi, inajionesha kweli,
Walihonga sana wapi, kafufuka Yesu kweli,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
9. Ni msingi wa Kanisa, kafufuka kweli kweli,
Tuishio ni hamasa, hii imani halali,
Kuwa hai Yesu fursa, kumwamini huyu kweli,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
10. Usiyemwamini Yesu, kafufuka kweli kweli,
Yuko hai huyu Yesu, mwana wake Mungu kweli,
Hukumu inamhusu, ataja hukumu kweli,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
11. Hanao mfano wake, mwana wake Mungu kweli,
Kwanza kuzaliwa kwake, na wanadamu ni mbali,
Kufa kufufuka kwake, yeye ni adhimu mali,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
12. Kama wewe wamwamini, mkazi kwake halali,
Na endapo humwamini, kwake kutakuwa mbali,
Sasa akili kichwani, vema uishike kweli,
Kafufuka kweli kweli, shangilia Haleluya.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
Leo Aprili 2,2026.