ISTANBUL-Wajumbe wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) wamemchagua Balozi Anda Filip wa Romania kuwa Katibu Mkuu wake wa tisa katika Mkutano Mkuu wa 152 uliofanyika Istanbul, Türkiye, hatua ya kihistoria baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya miaka 140 ya taasisi hiyo.
Filip alishinda kwa kishindo baada ya kupata kura 229 kati ya 321 zilizopigwa katika uchaguzi huo wa Jumapili.
Ameshinda dhidi ya wagombea wengine wenye uzoefu mkubwa kutoka sekta za diplomasia, sheria za kimataifa, mabunge na Umoja wa Mataifa, katika ushindani mkali wa kimataifa.
Matokeo yalionesha Dionysia-Theodora Avgerinopoulou wa Ugiriki akipata kura 47, Cecilia Widegren wa Sweden kura 29, Fatou Dieng Thiam kura 14, huku Filip akiongoza kwa 229.
Filip anachukua nafasi ya Martin Chungong, ambaye alihudumu tangu 2014 na kumaliza miaka yake ya uongozi Juni 2026.
Akiwa na zaidi ya miaka 20 ndani ya IPU, Filip amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za kidiplomasia na uongozi katika Umoja wa Mataifa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Romania.

