Maafisa Ardhi mahakamani Hanang' kwa tuhuma za rushwa

NA DIRAMAKINI

MAAFISA wawili wa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi yanayohusiana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Shauri hilo la jinai lenye namba 7891/2026 limefunguliwa Aprili 14, 2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Hanang’, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mheshimiwa Arnold Kileo.

Washtakiwa katika shauri hilo ni Bw. Erick Erasmus Mbeya na Bw. Egidius Sweetber Kashaga, wote wakiwa watumishi wa umma katika idara ya ardhi ya halmashauri hiyo.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, toleo la mwaka 2023. Inadaiwa kuwa, wakiwa katika nafasi zao za utumishi wa umma, walitumia vibaya mamlaka waliyopewa kwa manufaa yasiyostahili.

Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Hanang’, Bw. Daudi Kingazi aliieleza mahakama kuwa,washtakiwa walihusika katika kuhamisha umiliki wa kiwanja, kukisajili upya na hatimaye kutoa hati ya umiliki kwa mtu mwingine, kinyume na taratibu za kisheria.

Alibainisha kuwa, vitendo hivyo vinakiuka kifungu cha 187(1)(d)(i) cha Sheria ya Ardhi, Sura ya 113.

Baada ya kusomewa hati ya mashtaka, washtakiwa wote walikana kutenda makosa yanayowakabili.

Hata hivyo, walikidhi masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama, hivyo wapo nje kwa dhamana wakisubiri kuendelea kwa taratibu za kisheria.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 5, 2026, ambapo itatajwa tena kwa ajili ya kusomwa kwa hoja za awali (preliminary hearing).

Hatua hiyo inaakisi juhudi zinazoendelea za vyombo vya dola katika kuhakikisha uwajibikaji na kupambana na vitendo vya rushwa ndani ya utumishi wa umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here