TEF yatamani kuona mabadiliko chanya uchumi wa vyombo vya habari na wanahabari

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ametoa wito kwa wadau wa tasnia ya habari nchini na duniani kwa ujumla kuanza tafakuri ya kina kuhusu mikakati madhubuti ya kuimarisha uchumi wa vyombo vya habari pamoja na wanahabari.
Balile ameyasema hayo leo Aprili 16,2026 katika mkutano maalum wa wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, mkutano huo pamoja na mingine ijayo unapaswa kuwa chachu ya kuibua suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Vilevile, Balile amefanua kuwa, tasnia ya habari duniani inakabiliwa na misukosuko mbalimbali, ikiwemo kupungua kwa mapato ya vyombo vya habari, mabadiliko ya kiteknolojia, pamoja na mazingira magumu ya kazi kwa wanahabari, hali inayochangia kudhoofisha ufanisi wa utendaji wao.

“Ni wajibu wetu sasa kutafakari kwa kina na kubuni mikakati endelevu itakayohakikisha kuwa uchumi wa vyombo vya habari na wanahabari unaimarika."

Pamoja na changamoto hizo,Balile amebainisha kuwa, katika miaka ya karibuni, tasnia ya habari nchini imeonesha dalili za kuimarika katika baadhi ya maeneo.

Hata hivyo, Balile ametoa msisitizo kwa wanahabari kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma yao ili kulinda hadhi na uaminifu wa vyombo vya habari.

Kwa upande mwingine, Balile ameeleza kuwa, hali ya uchumi wa wanahabari wengi, ndani na nje ya Tanzania, imeendelea kuyumba kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya kiuchumi katika uzalishaji wa maudhui ya habari.

Ameongeza kuwa nchini Tanzania, baadhi ya magazeti tayari yamelazimika kusitisha shughuli zake, huku vyombo vingine vya habari zikiwemo runinga na redio, vikikabiliwa na changamoto za uendeshaji zinazoathiri uthabiti wao kifedha.

Mkutano huo wa TEF pia unajadili mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya jukwaa hilo, ambapo wanachama wanapata fursa ya kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha uendeshaji na ufanisi wa taasisi hiyo muhimu katika tasnia ya habari nchini.

Wito wa TEF unatazamwa kuwa hatua muhimu katika kuchochea mjadala mpana kuhusu mustakabali wa tasnia ya habari na ustawi wa wanahabari katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here