Maandalizi ya AFCON 2027 yashika kasi, Waziri Mkuu ataja mafanikio Sekta ya Michezo nchini

DODOMA-Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, Serikali itaendelea kusimamia na kuratibu ushiriki wa Tanzania katika michezo ya kimataifa sambamba na kuharakisha maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027 kwa lengo la kujenga urithi endelevu wa michezo, uchumi na heshima ya Taifa.
Ameyasema hayo Aprili 1,2026 wakati akiwasilisha hotuba yake kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma.

Amesema,Tanzania inaendelea na maandalizi ya kuwa mwenyeji katika mashindano ya AFCON 2027, ambayo yanahusisha ujenzi na ukarabati wa viwanja pamoja na miundombinu wezeshi ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Arusha uliofikia asilimia 75.

“Ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa umefikia asilimia 95; na ujenzi wa Uwanja wa Dodoma umefikia asilimia nne. Vilevile, Serikali imekamilisha ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Meja Jenerali Isamuhyo, Gymkhana Club na Shule ya Sheria Tanzania kwa ajili ya mazoezi.”

Aidha, Waziri Mkuu amesema,Serikali inaendelea na ujenzi wa Viwanja vya Farasi, Gymkhana Annex na Leaders Club ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha miundombinu ya michezo nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema, mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya michezo yanatokana na uwekezaji wa kimkakati na uongozi thabiti wa Serikali.

“…Ninapenda kutumia fursa hii pia, kulipongeza Shirikisho la Mchezo wa Mpira wa Miguu Tanzania kwa uongozi, uratibu na usimamizi mzuri wa mchezo huo hapa nchini. Kupitia uongozi huo, kwa mara ya kwanza Tanzania imefanikiwa kuingiza vilabu vinne kwa pamoja katika hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Bingwa na Shirikisho Barani Afrika.”

Waziri Mkuu amevitaja vilabu hivyo kuwa ni Klabu ya Michezo Yanga (wananchi), Klabu ya Michezo Simba (wenye nchi), Klabu ya Michezo Azam (wana lambalamba) na Klabu ya Michezo Singida (wana kilemankundi).

Amesema kuwa,mafanikio katika mchezo wa mpira wa miguu na michezo mingine kwa ujumla ni matokeo ya uwekezaji na hamasa inayotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mafanikio hayo, siyo tu yanaleta burudani kwa mashabiki, bali yanatoa fursa ya ajira na uwekezaji hapa nchini.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuimarisha ushiriki wa wanafunzi katika michezo ili kuibua na kukuza vipaji vyao, ikiwa ni mkakati wa muda mrefu wa kujenga kizazi cha wanamichezo wenye ushindani kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here