Mahitaji ya usafiri wa anga yaongezeka duniani,ndege kubwa zatawala soko la abiria

NA DIRAMAKINI

NI wazi kuwa,mahitaji ya usafiri wa anga duniani yanaendelea kuimarika mwaka 2026, huku mashirika ya ndege yakielekeza uwekezaji wao katika ndege kubwa.
Ni ndege zenye uwezo mkubwa wa kubeba abiria wengi pamoja na ufanisi wa matumizi ya mafuta.

Takwimu za hivi karibuni kutoka International Air Transport Association (IATA) za Januari 2026 zinaonesha kuwa, idadi ya abiria wa anga imeongezeka kwa asilimia 3.8 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Kutokana na ongezeko hilo la mahitaji, uchambuzi wa Simple Flying umeainisha ndege sita zinazoongoza kwa uwezo mkubwa wa kubeba abiria katika safari za kibiashara duniani kwa sasa.

Katika nafasi ya kwanza, Airbus A380-800 inaendelea kushika rekodi ya kuwa ndege kubwa zaidi ya abiria duniani.

Ndege hii yenye tabaka mbili kamili ina uwezo wa kubeba hadi abiria 853. Hata hivyo, mashirika mengi ya ndege, yakiwemo Emirates, hupunguza idadi hiyo hadi kati ya abiria 489 na 555 ili kuboresha nafasi na faraja kwa wasafiri.

A380 imeendelea kuwa mhimili muhimu katika njia zenye msongamano mkubwa kama vile kati ya Dubai na London nchini Uingereza .

Nafasi ya pili inashikiliwa na Boeing 747-400, maarufu kama Malkia wa Anga.Ndege hii ina uwezo wa juu wa kubeba hadi abiria 660, ingawa muundo wa kawaida wa daraja tatu hubeba takribani abiria 416.

Kwa miongo kadhaa, 747-400 imekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza gharama za usafiri wa kimataifa na kuleta mapinduzi katika sekta ya anga.

Katika nafasi ya tatu ni Boeing 777-300ER, yenye uwezo wa kubeba hadi abiria 550. Kwa kawaida hubeba kati ya abiria 350 hadi 400, na imejipatia umaarufu katika safari ndefu kutokana na uwezo wake wa kusafiri umbali wa hadi maili 7,300 pamoja na matumizi ya injini zenye nguvu aina ya GE90.

Nafasi ya nne inachukuliwa na Boeing 747-8 Intercontinental, ambayo ndiyo ndege ndefu zaidi ya abiria kibiashara duniani.

Ina uwezo wa kubeba hadi abiria 605, ingawa muundo wa kawaida hubeba takribani abiria 467.

Licha ya uwezo wake mkubwa, ndege hii imebaki kuwa adimu kutokana na idadi ndogo ya mashirika ambapo ni takribani 48 pekee ndiyo yaliyonunua toleo lake la abiria.

Katika nafasi ya tano ni Airbus A350-1000, yenye uwezo wa kubeba hadi abiria 480.

Hii ndiyo toleo kubwa zaidi katika familia ya A350 na hutumika katika safari ndefu kama vile kati ya Doha na Auckland.

Ndege hii inachukuliwa kama mbadala wa kisasa wa A380 kutokana na ufanisi wake mkubwa wa matumizi ya mafuta na gharama ndogo za uendeshaji.

Nafasi ya sita inakamilishwa na Airbus A330-900neo, yenye uwezo wa kubeba hadi abiria 460, ingawa kwa kawaida hubeba takribani abiria 310.

Ndege hii ni mshindani wa moja kwa moja wa Boeing 787-9, na imeundwa kwa kutumia takribani asilimia 95 ya muundo wa A330ceo, hatua inayosaidia kupunguza gharama za matengenezo kwa mashirika ya ndege.

Pamoja na ongezeko la uwezo wa ndege hizi, wataalamu wa anga wanabainisha kuwa, mashirika mengi ya ndege hayatumii kikamilifu uwezo wa juu wa kubeba abiria.

Badala yake, huweka kipaumbele katika mipangilio ya viti inayotoa nafasi zaidi, faraja na huduma bora kwa wasafiri, jambo linaloendana na ushindani wa kibiashara na matarajio ya wateja katika soko la kimataifa la usafiri wa anga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here