Mbunge Bashungwa hajaridhishwa na mabadiliko ya Stendi za Kayanga na Omurushaka jimboni Karagwe

KAGERA-Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameonesha hali ya kutoridhishwa na utekelezaji wa maamuzi ya mabadiliko ya matumizi ya stendi za mabasi na magari mengine katika Wilaya ya Karagwe na kueleza kuwa kuwa mwongozo huo haukushirikisha wadau na unatekelezwa kwa kutumia nguvu, hali inayowaumiza wananchi.
Akizungumza Aprili 04, 2026 wakati akituma salamu za Pasaka kwa wananchi wa Jimbo la Karagwe, Bashungwa amesema maamuzi yaliyofanywa hayakuwashirikisha wananchi wala wasafirishaji, jambo lililosababisha malalamiko na changamoto katika utekelezaji wake.

Kutokana na hali hiyo, Bashungwa ametaka kurejeshwa kwa utaratibu wa awali wa matumizi ya stendi za Kayanga na Omurushaka wakati inatafuwa suluhisho linalokubalika kwa pande zote na kueleza kuwa kabla ya mabadiliko hayo hapakuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Masuala haya hayahitaji matumizi ya nguvu, bali yanahitaji ushirikishwaji wa wananchi na wadau wa usafirishaji. Tutumie busara na kukaa pamoja tutapata suluhisho linalokubalika bila kuwaumiza wananchi wala kuongeza usumbufu usio wa lazima,” amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amewataka Viongozi wa Wilaya ya Karagwe wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Julius Laizer, pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Longino Rwenduru kutumia hekima na busara kwa kushirikisha wananchi na wadau wa usafirishaji ili kumaliza changamoto hiyo.

Katika kuelekea suluhisho la kudumu, Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais, Dkt,. Samia Suluhu Hassan amesikia maombi ya Wanakaragwe aliyoyatoa katika mkutano wa kampeni ambapo Serikali imepanga kutenga Bajeti ya shilingi Bilioni 5.5 kwa ajili ya ujenzi wa stendi mpya ya kisasa ya Kishao.

Kadhalika, Bashungwa ameonesha kutoridhishwa na matumizi ya nguvu katika utekelezaji wa maamuzi hayo, akieleza kuwa hatua hizo zimekuwa chanzo cha kero, manung’uniko na hata kuwaingiza baadhi ya wananchi katika hali ngumu ya kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here