NA DIRAMAKINI
MFANYABIASHARA mmoja jijini Arusha, Bi. Antilda Method Kahumuliza amehukumiwa kulipa faini ya Shilingi 100,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kughushi leseni ya biashara.
Hukumu hiyo ilitolewa Aprili Mosi, 2026 na Mahakama ya Wilaya ya Arusha mbele ya Hakimu Mkazi, Mheshimiwa Harrieth Marando, katika shauri la jinai namba 7173/2026, lililoendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Bw.Melvin Richard.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa alikabiliwa na kosa la kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023. Ilidaiwa mahakamani kuwa, akiwa mfanyabiashara katika Mkoa wa Arusha, Bi. Kahumuliza alighushi leseni ya biashara kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa alikiri kosa bila shuruti, hatua iliyoiwezesha mahakama kumtia hatiani mara moja.
Akitoa hukumu, Mheshimiwa Marando aliamuru mshtakiwa kulipa faini ya Shilingi 100,000 au, mbadala wake, kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani. Hata hivyo, mshtakiwa alitekeleza adhabu ya faini na hivyo kuepuka kifungo.
Kesi hiyo inatoa onyo kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa biashara, ikiwemo matumizi sahihi ya nyaraka halali.
Tags
Habari
Kughushi Leseni ya Biashara
Mahakamani Leo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
