Moduli ya Rufaa kuboresha mnyororo wa ugavi

DODOMA-Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema ujenzi wa moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST utachangia kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi kwenye mnyororo wa ugavi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), (Katikati Kulia), akiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), na viongozi wengine wakisikiliza maelezo kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando (kushoto), kuhusu mchango wa PPAA katika Mnyororo wa Ugavi, wakati Mhe. Waziri Mkuu alipotembelea banda ya maonesho katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma, kabla ya kuzindua rasmi Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025.

Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando amebainisha hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 na kuongeza kuwa Moduli hiyo imewaunganisha wazabuni wote na Taasisi nunuzi nchini ili kuongeza uwajibikaji katika utatuzi wa migogoro inayotokana na michakato ya ununuzi wa umma.

“PPAA ni moja kati ya taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini, matumizi ya moduli hiyo katika mnyororo wa ugavi yatachangia kutoa maamuzi kwa haki na wakati na kuwezesha miradi ya Serikali kutekelezwa kwa wakati uliokusudiwa,” amesema Bw. Sando.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), akizindua rasmi Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando amebainisha kuwa matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika ununuzi wa umma yatasaidia kuongeza uwazi, kupunguza gharama, kuokoa muda, utunzaji wa nyaraka na hivyo kuongeza ufanisi katika hukumu zinazotolewa kutokana na michakato mbalimbali ya zabuni za umma.

Bw. Sando ameongeza kuwa, PPAA imefanikiwa kushiriki katika utungwaji wa Sera ya Taifa ya Mnyororo wa Ugavi, Sheria ya Ununuzi wa Umma, Kanunuzi za Ununuzi wa Umma na Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma ambapo yote ni michango wa Mamlaka ya Rufani katika mnyororo wa ugavi.

Kadhalika, Mamlaka ya Rufani inatarajia kuboresha kipengele cha makundi maalum na vijana ambapo inategemea kuboresha gharama au tozo za kesi kwa makundi maalum pamoja na kuelekeza nguvu kwa vijana na kuhakikisha wanapata fursa ya kudai haki zao katika michakato ya ununuzi wa umma.

Awali akizindua Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amezielekeza mamlaka, taasisi na wadau wote wanaosimamia utekelezaji wa Sera hiyo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwazi na utawala wa sheria.‎
Sehemu ya viongozi mbalimbali walioshiriki katika uzinduzi wa Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo wakati akizundua Sera hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dkt. Nchemba amesema changamoto zinazoikumba sekta ya ununuzi wa umma hazitokani na sera au sheria zilizopo, bali ni uzembe na mitazamo ya baadhi ya watendaji.‎

‎Ameongeza kuwa taarifa za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) zinaonesha wazi kuwa kasoro nyingi zinasababishwa na utekelezaji dhaifu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

“Sehemu kubwa ya changamoto hizo zinatokana na hulka, tabia na mitazamo ya watendaji. Hivyo, ni lazima tubadilike ili kufikia malengo ya sera hii,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Aidha, Waziri Mkuu, amezitaka wizara, taasisi na mamlaka zote kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni zinazokinzana na sera hiyo ili kuweka mazingira rafiki ya utekelezaji wake.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), akizungumza na viongozi wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), wakati alipotembelea banda ya maonesho katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma, kabla ya kuzindua rasmi Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025.

Naye Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema sera hiyo ni mwongozo muhimu utakaosaidia kuimarisha mifumo ya ugavi katika sekta ya umma, kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kudhibiti vitendo vya rushwa.‎

Balozi Khamis ameongeza kuwa utekelezaji wa sera hiyo utaongeza ajira, kuimarisha mnyororo wa thamani na kuchochea mageuzi makubwa ya kiuchumi kuelekea dira ya maendeleo ya mwaka 2050.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here