NA DIRAMAKINI
IDADI ya watu waliopoteza maisha kufuatia mvua kubwa zilizoikumba nchi ya Angola katika siku za hivi karibuni imeongezeka na kufikia zaidi ya 30, kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizoripotiwa leo Jumanne.
Mvua hizo kubwa zilisababisha mafuriko ya ghafla yaliyosomba makazi ya watu, kuharibu miundombinu na kujaa maji katika mitaa ya mji mkuu Luanda pamoja na mji wa Benguela uliopo katika pwani ya Bahari ya Atlantiki.
Rais wa Angola, João Lourenço amesema kuwa, taifa hilo linakabiliwa na changamoto kubwa katika juhudi za kuwaokoa manusura, kuwatafuta waliopotea na kutoa huduma za matibabu kwa waathirika wa janga hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali zilizotolewa Jumapili, idadi ya vifo ilikuwa 15 huku maelfu ya wananchi wakilazimika kuyahama makazi yao kutokana na athari za mafuriko hayo.
Hata hivyo, takwimu mpya zinaonesha ongezeko kubwa la vifo kadri juhudi za uokoaji zinavyoendelea.
Mji wa Benguela umetajwa kuathirika zaidi, ambapo watu 23 wamepoteza maisha, wakati katika mji wa Luanda watu sita wamethibitishwa kufariki na mmoja kuripotiwa kupotea, kwa mujibu wa vyombo vya zimamoto.
Wakati huo huo, katika nchi jirani ya Namibia, kiwango cha maji katika Mto Zambezi kimeongezeka kwa kasi, na kuwalazimu maelfu ya wakazi walioko kandokando ya mto huo kuhama makazi yao.
Inaelezwa kuwa, kina cha maji kimefikia takribani mita 6.8, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya wastani wa kawaida wa mita nne.
Ingawa mvua kubwa ni jambo la kawaida katika ukanda wa Kusini mwa Afrika wakati wa msimu wa mvua, wataalamu wa sayansi wanaonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na shughuli za binadamu yanaongeza uwezekano, muda na ukali wa matukio kama hayo ya hali mbaya ya hewa.
Kwa sasa, mamlaka zinaendelea na juhudi za uokoaji huku zikitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari zaidi ili kuepuka madhara zaidi yanayoweza kujitokeza.(AFP/BSS).
