DODOMA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari leo Aprili 14,2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Taasisi ya Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), Mhe. Balozi Wilson K. Masilingi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bungeni jijini Dodoma.
Katika kikao hicho chenye lengo la kuimarisha mahusiano ya kikazi na ushirikiano wa taasisi, Mhe. Balozi Masilingi amemtembelea Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kufuatia uteuzi wake, pamoja na kumpongeza kwa namna anavyotekeleza kwa ufanisi jukumu la kuishauri Serikali katika masuala ya kisheria nchini.Mhe. Balozi Masilingi aliteuliwa kushika wadhifa huo Januari 29, 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo tangu uteuzi wake ameanza ziara za kikazi kwa lengo la kujenga na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta husika.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamejadili kwa kina mbinu na mikakati ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TEITI, hususan katika kukuza uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za madini,mafuta na gesi asilia nchini.
Aidha,pande zote mbili zimesisitiza umuhimu wa ushirikiano endelevu kati ya taasisi za umma katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinasimamiwa kwa manufaa ya wananchi, sambamba na kuzingatia misingi ya kisheria na uwazi.Katika ziara hiyo, Mhe. Balozi Masilingi aliambatana na Katibu Mtendaji wa TEITI, Bi. Mariam Mgaya.











