NECTA yatangaza Ratiba ya Upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne Oktoba,2026

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA), chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, limetangaza rasmi ratiba ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne kwa mwaka 2026, utakaoanza tarehe 21 Oktoba hadi 22 Oktoba 2026. 
Ratiba hiyo inaainisha masomo mbalimbali yatakayofanyiwa tathmini pamoja na muda maalum wa kila somo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupima ufanisi wa ujifunzaji katika elimu ya msingi.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, siku ya kwanza ya upimaji, Jumatano tarehe 21 Oktoba 2026, itaanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi kwa somo la Jiografia na Mazingira: Sanaa na Michezo (Geography and Environment: Arts and Sports). Baada ya hapo, wanafunzi watapata mapumziko ya saa moja kuanzia saa 3:30 hadi saa 4:30 asubuhi.

Upimaji utaendelea saa 4:30 hadi saa 6:00 mchana kwa somo la Hisabati, likifuatiwa na mapumziko marefu kuanzia saa 6:00 hadi saa 8:00 mchana. 

Hatimaye, siku hiyo itahitimishwa kwa somo la Sayansi litakalofanyika kuanzia saa 8:00 hadi saa 9:30 mchana.

Siku ya pili, Alhamisi tarehe 22 Oktoba 2026, wanafunzi wataanza na somo la Kiswahili kuanzia saa 2:00 hadi saa 3:00 asubuhi. 

Baada ya mapumziko ya saa moja kuanzia saa 3:00 hadi saa 4:00 asubuhi, watafanya mtihani wa Kiingereza kuanzia saa 4:00 hadi saa 5:00 asubuhi.

Ratiba inaonyesha pia vipindi vya mapumziko kati ya masomo, ikiwemo mapumziko ya saa 5:00 hadi saa 5:30 asubuhi kabla ya mitihani ya lugha za kigeni. 

Kuanzia saa 5:30 hadi saa 6:30 mchana, wanafunzi watafanya mojawapo ya masomo ya lugha ya kigeni, ikiwemo Kifaransa, Kiarabu au Kichina, kulingana na mtaala wa shule husika.

Baada ya mapumziko ya ziada kuanzia saa 6:30 hadi saa 8:00 mchana, siku ya pili itahitimishwa kwa somo la Historia ya Tanzania na Maadili kuanzia saa 8:00 hadi saa 9:30 mchana.

Ratiba hii inalenga kuhakikisha wanafunzi wanapata muda wa kutosha kufanya mitihani yao kwa utulivu pamoja na vipindi vya kupumzika ili kuongeza umakini na ufanisi. 

Aidha,sasa ni jukumu la walimu, wazazi na wadau wa elimu kuhakikisha wanafunzi wanajiandaa ipasavyo kwa kuzingatia ratiba hiyo.

Upimaji wa Darasa la Nne ni hatua muhimu katika mfumo wa elimu nchini Tanzania, ukiwa na lengo la kupima umahiri wa wanafunzi katika masomo ya msingi na kutoa mrejesho kwa ajili ya kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya elimu ya msingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here