NA DIRAMAKINI
MVUTANO wa kisiasa na kijeshi katika eneo la Ghuba ya Uajemi umeendelea kuongezeka baada ya meli tatu za mizigo kushambuliwa Aprili 22,2026 kwa risasi katika Mlango wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.
Kwa mujibu wa taarifa za usalama wa baharini, meli hizo zililengwa kwa mashambulizi ya silaha za moto katika mazingira yanayoashiria kuongezeka kwa hatari kwa shughuli za usafirishaji katika eneo hilo nyeti.
Hata hivyo, ilithibitishwa kuwa wafanyakazi wote waliokuwa ndani ya meli hizo wako salama licha ya baadhi ya meli kupata uharibifu mdogo hadi mkubwa katika miundombinu yake.
Shirika la Uingereza linalosimamia Usalama wa meli Baharini (UKMTO) limeeleza kuwa,angalau moja ya meli hizo ilikaribiwa na chombo cha kijeshi kabla ya kufyatuliwa risasi pamoja na makombora ya kurushwa kwa mkono, hali iliyosababisha uharibifu mkubwa katika sehemu ya daraja la kuongozea meli.
Tukio hilo linajiri katika kipindi ambacho mvutano kati ya Iran na Marekani pamoja na washirika wake umeendelea kuwa mkubwa, licha ya kuwepo kwa juhudi za kidiplomasia za kusitisha mapigano.
Katika mazingira hayo, Iran kupitia Kikosi chake cha Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) imeripotiwa pia kukamata baadhi ya meli kwa madai ya kukiuka sheria za baharini, ikiwemo kutumia mifumo ya urambazaji isiyo halali.
Mlango wa Hormuz ni njia muhimu ya kimkakati inayobeba takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia duniani.
Hivyo, mashambulizi hayo yamezua hofu kubwa katika masoko ya kimataifa, hasa katika sekta ya nishati na biashara ya usafirishaji, huku bei za mafuta zikionesha dalili za kupanda zaidi kutokana na hatari ya kukwamishwa kwa usafirishaji.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema kuwa,matukio hayo yanaashiria hatari ya kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama katika eneo hilo, jambo linaloweza kuathiri uchumi wa dunia iwapo hatua za haraka za kidiplomasia hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo.(NA)
