Rais Dkt.Mwinyi ateua wakuu wa wilaya

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, hatua inayolenga kuimarisha utendaji wa Serikali katika ngazi za wilaya na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 10,2026 na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi Zena A. Said.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dkt. Said Haji Mrisho ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Unguja.

Kabla ya uteuzi huo, alikuwa akihudumu kama Katibu Tawala wa Wilaya ya Mjini, nafasi iliyompa uzoefu mpana katika masuala ya utawala wa umma.

Naye Lailah Burhan Ngozi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A”, Unguja. Lailah, ambaye ana taaluma ya uuguzi, pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa na uzoefu katika shughuli za kijamii na kisiasa.

Aidha, Ali Abdalla Said Natepe ameteuliwa kushika wadhifa wa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B”, Unguja.

Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi, akijihusisha na uratibu wa shughuli za kiutawala katika ngazi ya mkoa.

Kwa upande wake, Riziki Daniel Yussuf ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A”, Unguja.

Kabla ya hapo, alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

Vilevile, Zuhura Mgeni Othman ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Pemba.

Kabla ya uteuzi huo, aliwahi kuwa Ofisa Mdhamini katika Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Pemba, ambapo alipata uzoefu katika usimamizi wa sekta ya utalii na urithi wa kihistoria.

Uteuzi huo unaanza rasmi leo Aprili 10, 2026 ambapo wateule wote wanatarajiwa kuapishwa Aprili 13, 2026 saa 4:00 asubuhi katika Ikulu ya Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here