NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya moto ulioteketeza Soko la Mawasiliano (Simu 2000) lililopo katika Kata ya Sinza, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, tarehe 04 Aprili, 2026, majira ya saa kumi na moja jioni.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 5,2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S.Machumu.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, moto huo ulianza katika vizimba vya kuuzia nguo kabla ya kusambaa katika maeneo mengine ya biashara, yakiwemo maduka ya vyombo na bidhaa mbalimbali, huku jitihada za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zikiendelea kudhibiti hali hiyo.
Rais Dkt. Samia ametoa pole kwa wafanyabiashara waliopoteza mali zao, na wananchi na wateja watakao koswa huduma kufuatia tukio hilo.
Aidha, ameziagiza mamlaka za uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo, kufanya tathmini ya madhara na hasara iliyotokea, na kuchukua hatua stahiki haraka.
