NA DIRAMAKINI
RAIS wa Kenya, Dkt. William Ruto anatarajiwa kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 5 Mei 2026, katika tukio linalotarajiwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili jirani ya Afrika Mashariki.
Taarifa hiyo ilitolewa rasmi Aprili 29, 2026 na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo alipokuwa akisoma tangazo la Katibu wa Bunge mbele ya wabunge wakati wa kikao kinachoendelea jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, hotuba ya Rais Ruto itakuwa sehemu muhimu ya shughuli za siku hiyo, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na wadau wa maendeleo.
Ujio wa Rais Ruto unalenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kikanda kati ya Tanzania na Kenya, hususan katika nyanja za biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi.
Pia,hatua hiyo inaakisi dhamira ya pamoja ya nchi hizo mbili katika kukuza ustawi wa wananchi wao kupitia ushirikiano wa karibu na endelevu.
Hotuba ya Rais Ruto inatarajiwa kugusa masuala mbalimbali ya kimkakati yanayohusu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwemo kuondoa vikwazo vya kibiashara, kuimarisha miundombinu ya pamoja, pamoja na kukuza fursa za uwekezaji katika sekta muhimu za uzalishaji.
Tangazo hilo limetolewa wakati wa Kikao cha 19 cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 13, unaoendelea jijini Dodoma, ambapo masuala mbalimbali ya kitaifa yanaendelea kujadiliwa na kuamuliwa na chombo hicho kikuu cha kutunga sheria nchini.
Vilevile, ujio wa Rais Ruto unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha mahusiano ya kihistoria kati ya Tanzania na Kenya, huku ukifungua ukurasa mpya wa ushirikiano wenye tija kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
