NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameongoza mamia ya mashabiki wa soka kushuhudia fainali ya michuano ya Ligi ya Muungano 2026 iliyowakutanisha wapinzani wakubwa, Simba Sports Club na Young Africans Sports Club (Yanga) katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi, Aprili 29, 2026.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali na kusisimua kwa muda wote, Simba iliibuka mabingwa baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1–0 dhidi ya Yanga.
Bao pekee la ushindi lilifungwa na kiungo Selemani Mwalimu katika dakika ya 120 ya mchezo, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za kawaida.
Katika hafla hiyo,Rais Dkt.Mwinyi alimkabidhi nahodha wa Simba, Shomari Kapombe kombe la ubingwa pamoja na hundi ya shilingi milioni 150 kama zawadi ya ushindi.
Kwa upande mwingine, timu ya Yanga ilikabidhiwa hundi ya shilingi milioni 100 baada ya kumaliza katika nafasi ya pili, huku nahodha wao Bakari Mwamnyeto akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya kikosi.
Michuano hiyo ya Ligi ya Muungano 2026 ilishirikisha jumla ya timu nane, zikiwemo nne kutoka Zanzibar ambazo ni Muembe Makumbi, Mlandege FC, KVZ FC na Mafunzo FC, pamoja na nne kutoka Tanzania Bara ambazo ni Simba, Singida Big Stars, Azam FC na Yanga.
Mashindano hayo yaliandaliwa mahsusi katika kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yakilenga kukuza mshikamano wa kitaifa kupitia michezo.
Aidha, fainali hiyo ilibeba dhima ya kuwaenzi waasisi wa Muungano huo, ambao ni Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Julius Kambarage Nyerere pamoja na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.
Kwa ujumla, fainali hiyo imeacha kumbukumbu ya kipekee katika historia ya soka nchini, ikionesha mchango mkubwa wa michezo katika kuimarisha umoja, amani na utambulisho wa kitaifa.
