DODOMA-Wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoiwakilisha nchi kwenye Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), wamesisitizwa kuhakikisha kuwa uwakilishi wao unakwenda sambamba na misingi ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 ili kutetea na kulinda maslahi mapana ya taifa.
Msisitizo huo umetolewa Aprili 2, 2026, kwenye Ofisi za Bunge jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja kati ya Wizara na wawakilishi hao kilichoongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Sillo (Mb).
Akiwasilisha mada maalum kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mikakati na Siasa za Ulimwengu, Balozi Thobias Makoba, amewasisitiza wajumbe hao kuoanisha vipaumbele vya Tanzania na kauli mbiu ya mkutano ujao isemayo ‘Kustawisha Matumaini, Kulinda Amani na Kuhakikisha Haki kwa Kizazi Kijacho’.
Amebainisha kuwa,wawakilishi hao wanapaswa kuipa kipaumbele Diplomasia ya Uchumi na msimamo wa nchi wa kutofungamana na upande wowote wakati wa Mkutano wa 152 wa IPU utakaofanyika jijini Instanbul Uturuki kuanzia tarehe 15 hadi 18 Aprili. 2026.
Vilevile, walihimizwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya 2050 wakati wa ushiriki wao katika Mkutano huo wa 152 wa IPU.
Aidha, Balozi Makoba amesema mkutano huo utumike kuitangaza Tanzania kama nchi inayozingatia misingi ya haki na usalama, mambo ambayo ni nguzo kuu katika kuvutia uwekezaji na kutumia jukwaa hilo kuitangaza Tanzania kuelekea Mkutano wa 153 wa IPU unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha, Oktoba 2026.
Kwa upande wao, wawakilishi hao wameishukuru Wizara kwa mwongozo huo na kuahidi kuwa watahakikisha uwakilishi wao unalinda heshima ya nchi na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kinara wa diplomasia ya kibunge barani Afrika na duniani kote.











