PWANI-Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya, Prof. Tumaini Nagu amesema kuwa, Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Trilioni 1.34 kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma za afya msingi ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Prof. Nagu ameanisha kuwa, fedha hizo zimetumika kuboresha huduma za afya msingi kwa kujenga hospitali mpya zaidi 129, kukarabati hospitali kongwe 43, kuboresha vituo vya afya pamoja na kujenga vituo vya afya vipya zaidi ya 320, hivyo kuviwezesha kutoa huduma za uzazi wa dharura na huduma za dharura kwa watoto wachanga.
Prof. Nagu amesema hayo Aprili 29, 2026 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa 2026 yaliyofanyika Kibiti mkoani Pwani katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Zimbwini, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Prof. Nagu ameeleza kuwa, katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya msingi ambavyo ni hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati, Serikali imejenga miundombinu bora ya maji na unawaji wa mikono katika vituo 3,457 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Uimarishaji wa upatikanaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira (WASH) ambazo zinamfikia kila mwananchi popote alipo ni nguzo muhimu katika kudhibiti magongwa na ni kipaumbele cha Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesisitiza Prof. Nagu.
Prof. Nagu ameongeza kuwa Serikali imeendelea na jitihada zaidi ambapo katika mwaka wa fedha 2025/26 jumla ya vituo 505 vimepokea jumla ya Shilingi Bilioni 20.9 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji na usafi wa mazingira.
Sanjari na hilo, Prof. Nagu amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele cha kuboresha huduma katika sekta ya afya, pia amemshukuru Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa uongozi imara na usimamizi mzuri wa sekta ya afya unaowezesha kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza usawa wa upatikanaji wa huduma bora za afya msingi kwa wananchi.








