NA DIRAMAKINI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita imewafikisha mahakamani watumishi wa umma pamoja na wafanyabiashara wakikabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mirathi zinazozidi shilingi milioni 260.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na TAKUKURU, uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa watumishi sita wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita wanadaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa jumla ya shilingi 261,424,788.85.
Fedha hizo zilikuwa zimehifadhiwa katika akaunti ya mirathi ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita.
Inadaiwa kuwa,watumishi hao walishirikiana na wanufaika wanane wa mirathi hiyo, ambapo walikuwa wakiwashawishi kudai fedha zao kinyume cha utaratibu, kisha kuwalazimisha kurejesha sehemu ya fedha hizo kama hongo (maarufu kama “kickback”). Malipo hayo yalifanyika kwa njia ya miamala ya simu, fedha taslimu na mbinu nyingine zisizo rasmi.
Watuhumiwa wanaotajwa katika sakata hilo ni pamoja na watumishi wa mahakama hiyo ambao ni hakimu, maafisa na wasaidizi wa hesabu, karani pamoja na dereva.
Aidha, uchunguzi umebaini kuwepo kwa ushiriki wa watumishi kutoka taasisi nyingine za umma, wakiwemo watumishi wa halmashauri, sekta ya elimu ya juu, wizara pamoja na idara za ujenzi.
Pia, wafanyabiashara wanatajwa kuhusika katika mtandao huo wa ubadhirifu, wakishirikiana na watumishi hao katika kuratibu upatikanaji na mgawanyo wa fedha hizo kinyume cha sheria.
Kufuatia kukamilika kwa uchunguzi na kupatikana kwa kibali cha kuendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), watuhumiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita leo Aprili 30, 2026 na kusomewa mashitaka matano ya uhujumu uchumi yenye namba ECO.9295/2026 hadi ECO.9299/2026.

