Serikali kuendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu kodi ya asilimia 30 usafirishaji wa mazao ya misitu nje ya nchi

DODOMA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema,Serikali itaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu kodi ya asilimia 30 kwenye usafirishaji wa mazao ya misitu nje ya nchi ili kuhakikisha inalinda viwanda vya ndani bila kudhoofisha ukuaji wake.
Alisema hayo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Timida Mpoki kwa niaba ya Mbunge wa Mafinga Mjini, Mhe. Dickson Nathan Lutevele, aliyetaka kufahamu iwapo Serikali iko tayari kufanya mapitio ya kodi hiyo kufuatia malalamiko ya wadau wa viwanda.

Mhe. Omar alisema kuwa Serikali haiwezi kufanya maamuzi ya haraka bila kufanya tathmini ya kina, kwani hatua ya kutoza kodi hiyo ilichukuliwa ili kulinda viwanda vya ndani dhidi ya upungufu wa malighafi.

“Mheshimiwa Spika, tulifanya marekebisho haya kwa makusudi kabisa ili kudhibiti usafirishaji wa mazao ya misitu yasiyoongezwa thamani na kuhakikisha viwanda vya ndani vinapata malighafi ya kutosha,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliongeza kuwa Serikali imeanza kupokea mrejesho kutoka kwa wadau mbalimbali unaoonesha kuwa baadhi ya viwanda vimeathirika na utekelezaji wa kodi hiyo.

“Ni kweli kuna viwanda, hususan vile vya kati, vinaathirika. Serikali inalichukua jambo hili kwa uzito na ndiyo maana tunaendelea kufanya tathmini ya kina,” alisisitiza.

Alibainisha kuwa kupitia Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Serikali itaangalia kwa kina athari za kodi hiyo kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho.

“Endapo itabainika kuwa kodi hii inaleta madhara zaidi kuliko faida, Serikali haitasita kufanya marekebisho stahiki ili kulinda uwekezaji na ajira,” aliongeza Mhe. Balozi Omar.

Akijibu swali la msingi, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa kabla ya marekebisho ya sheria, kulikuwa na usafirishaji mkubwa wa mazao ya misitu nje ya nchi yasiyochakatwa au yaliyochakatwa kidogo, hali iliyosababisha upungufu wa malighafi kwa viwanda vya ndani.

Alifafanua kuwa, mwaka 2025 Serikali ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Usafirishaji Bidhaa Nje ya Nchi kwa kuweka ushuru wa asilimia 30 au kiwango maalum kwa kila kilo ya bidhaa kama veneer sheets ili kulinda viwanda vya ndani.

“Lengo lilikuwa ni kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani na kuhamasisha uongezaji thamani wa mazao ya misitu kabla ya kusafirishwa nje ya nchi,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, alikiri kuwa baadhi ya viwanda vilivyoathirika ni vile ambavyo havijafikia hatua za mwisho za uzalishaji wa bidhaa za misitu.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kufanya tathmini ili kuhakikisha hatua zilizochukuliwa zinaleta tija kwa sekta ya misitu na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here