NA DIRAMAKINI
SERIKALI kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kuimarisha huduma za mawasiliano katika Jimbo la Kasulu Vijijini mkoani Kigoma, kwa kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo ujenzi na ukamilishaji wa minara ya mawasiliano katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Maelezo hayo yametolewa Aprili 28, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kigoma vijijini Mhe. Edbily Kazala Kinyoma.Mhe. Dkt. Mkama ameeleza kuwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Serikali ilikamilisha ujenzi wa Mnara wa Mawasiliano mwaka 2014 katika Kata ya Helu ushingo kwa kushirikiana na Kampuni ya YAS Tanzania uliosaidia kuhudumia vijiji vya Seluhemebe na Helu.
Aidha, mwaka 2021, UCSAF kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ilijenga mnara mwingine katika Kijiji cha Mvinza, Kata ya Kengarakanda, huku mwaka 2025 mnara mwingine ukikamilika katika Kijiji cha Sogeeni Kwiriba, Kata ya St. Nyerere kupitia kampuni ya Vodacom Tanzania, hatua iliyoongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mhe. Dkt. Mkama aliongeza kuwa,pamoja na mafanikio hayo, Serikali kupitia UCSAF imepanga kutuma wataalam kufanya tathmini ya kina katika kata mbalimbali za Jimbo la Kasulu Vijijini ili kubaini mahitaji halisi ya mawasiliano.
Tathmini hiyo itasaidia kuainisha maeneo yenye uhitaji mkubwa na kuyaingiza katika mpango mkakati wa ujenzi wa minara ya mawasiliano kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.