WASHINGTON D.C-Serikali ya Italia imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya maendeleo hususan kilimo, maji na uzalishaji ili kuhakikisha inafikia malengo yake na wananchi kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Naibu Mkuu wa Kikosi Kazi cha Mpango wa Mattei (Mpango wa kimkakati wenye lengo la kubadilisha uhusiano kati ya Italia na Afrika kwa kuzingatia ushirikiano wa usawa badala ya mtazamo wa mfadhili na mpokeaji) katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Italia, Bw. Lorenzo Ortona, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, uliofanyika jijini Washington D.C nchini Marekani, pembezoni mwa Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Bw. Ortona amesema kuwa, kama ilivyo jukumu la ofisi yake, watahakikisha usimamizi wa Mpango wa Mattei unaongeza ushirikiano na Tanzania katika kutengeneza fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo kama kilimo, elimu, na afya.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Bw. Sosthenes Kewe, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Bw. Frank Nyabundege, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, na maafisa wengine wa Serikali na wajumbe wa Kikosi Kazi cha Mpango wa Mattei kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Italia.

