DODOMA-Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wamekumbushwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na kujituma ili kuhakikisha wanachangia kikamilifu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050, hususan katika maeneo ya sera, uratibu na usimamizi wa utekelezaji wake.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba J.A. Kabudi, wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo mara baada ya kuwasili rasmi na kupokelewa na uongozi na watumjshi wa Ofisi hiyo katika Jengo la Ngome jijini Dodoma tarehe 8 Machi, 2026.
Prof. Kabudi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na ubunifu miongoni mwa watumishi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
“Ni muhimu tushirikishane mawazo na kufanya kazi kwa pamoja ili kumsaidia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufanikisha adhima ya maendeleo yenye kuleta ustawi na furaha kwa Watanzania," alisema Prof. Kabudi.
Aliongezea kuwa upo umuhimu wa kushikamana ili kuendelea kuimarisha utendaji wetu ili kumwezesha Mheshimiwa Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Waziri Kabudi alibainisha kuwa mazingira ya kazi yenye mshikamano na mahusiano ya kifamilia hayapaswi kuwa chanzo cha uzembe au utovu wa nidhamu, bali yawe kichocheo cha kuongeza uwajibikaji na kufikia viwango vya juu vya utendaji.
Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi aliwataka watumishi kuendelea kumuombea aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi hiyo, Marehemu William Vangimembe Lukuvi, ili Mwenyezi Mungu amrehemu na kumpa pumziko la milele.
“Nitaendeleza, kadri nitakavyoweza, misingi na jitihada zilizoanzishwa na mtangulizi wangu katika kuijenga Ofisi hii,” aliongeza.
Awali, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Ummy Nderiananga, alimpongeza Prof. Kabudi kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kushika nafasi hiyo, akiahidi ushirikiano wa dhati kutoka kwa watumishi wote katika utekelezaji wa majukumu yake.








