NA DIRAMAKINI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa taarifa rasmi kwa wanachama wake waliochukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kikitaka wahusika hao kufika mbele ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa ajili ya kikao maalum cha usaili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao hicho kinatarajiwa kufanyika Aprili 24, 2026, saa 2:00 asubuhi, katika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ni sehemu ya mchakato wa chama katika kuwachuja na kuwathibitisha wagombea wanaowania nafasi hizo katika ngazi ya kikanda.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, ni wajibu wa kila mhusika kufika katika kikao hicho akiwa na kadi halali ya uanachama wa CCM pamoja na vyeti vyake halisi vya taaluma kwa ajili ya uhakiki.
Aidha, chama kimesisitiza kuwa gharama zote za usafiri na malazi zitabebwa na wahusika wenyewe bila msaada kutoka chama.
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi, maandalizi ya kikao hicho yamekamilika, na chama kinatarajia kupata wawakilishi wenye sifa stahiki watakaoweza kuiwakilisha vyema Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki.
CCM imewahimiza wahusika wote kuzingatia muda na masharti yaliyotolewa ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia kanuni na taratibu za chama.
