KILIMANJARO-Mahakama ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro Aprili 2, 2026 imewatia hatiani watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya uhujumu uchumi yaliyosababisha hasara kwa Serikali.
Washtakiwa hao ni Mohamed Khalfan Bakari, aliyekuwa Mhasibu wa Mapato, pamoja na Laurent Abiud Mgonja, aliyekuwa Mkusanya Ushuru katika halmashauri hiyo.
Mahakama imewahukumu kutumikia kifungo cha nje cha miezi kumi na miwili (12) sambamba na amri ya kurejesha fedha walizobainika kuzitumia kinyume cha sheria, kiasi cha Shilingi milioni 12 za Kitanzania.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani Novemba 27, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi, Mheshimiwa Elibahati Petro, wakikabiliwa na mashitaka matatu yanayohusiana na matumizi mabaya ya madaraka, ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma, pamoja na kuisababishia Serikali hasara.
Mashitaka hayo yaliwasilishwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (marejeo ya mwaka 2019), zikihusisha vifungu mbalimbali vinavyokataza matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kulinda uchumi wa taifa.
Ilielezwa mahakamani kuwa,fedha hizo zilipatikana kutokana na ukusanyaji wa ushuru wa mazao katika eneo la Makiwaru, ambapo washtakiwa walikuwa na wajibu wa kuziwasilisha katika akaunti rasmi ya halmashauri.
Hata hivyo, walishindwa kutekeleza wajibu huo na badala yake walizitumia kwa manufaa yao binafsi.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Suzan Kimaro, ambaye aliwasilisha ushahidi uliosaidia kuthibitisha hatia ya washtakiwa bila kuacha shaka.
Hukumu hiyo inatajwa kuwa ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za vyombo vya dola katika kuhakikisha uwajibikaji, uwazi, na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi nchini.
