Waziri Mkuu akagua Barabara ya Ntyuka hadi Kikombo jijini Dodoma

DODOMA-Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amekagua ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo yenye urefu wa kilomita 76 pamoja na kipande cha barabara ya Chololo–Mapinduzi (Makao Makuu ya TPDF) yenye urefu wa kilomita 5, katika Jimbo la Mvumi, Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma.
Mradi huu unaotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiwa na lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri, kuimarisha muunganiko kati ya Wilaya ya Dodoma Mjini na Chamwino, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo Hospitali ya Mvumi Mission.
Mradi huu unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 25 (ikiwemo Ntyuka–Mvumi–Makulu na Kikombo–Chololo–Mapinduzi) imefikia utekelezaji wa asilimia 80.9, na inatekelezwa na Mkandarasi M/s China Henan International Corporation Company Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 38.199.

Awamu ya pili yenye urefu wa kilomita 53 (Ntyuka–Mvumi Hospitali–Kikombo) imeanza kutekelezwa na Mkandarasi China First Highway Engineering Co. Ltd, ikiwa imefikia asilimia 5.2 ya utekelezaji kwa sasa, kwa gharama ya shilingi bilioni 98.488.
Aidha, mradi huu umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania ambapo zaidi ya wafanyakazi 500 wamehusishwa katika awamu zote mbili za ujenzi.

Taarifa ya utekelezaji wa mradi huo iliwasilishwa kwa Waziri Mkuu na Mhandisi Jefferson Nnko, ambapo alieleza hatua zilizofikiwa pamoja na changamoto na mikakati ya kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema: “Utekelezaji wa mradi huu ni dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia kuwaachia alama ya kudumu wakazi wa eneo hili, hii ni barabara muhimu sana kwa kuwa nimepita nimeona hili ni eneo la uzalishaji.”

Mheshimiwa Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa wakandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa kulingana na makubaliano ya mkataba.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa maagizo kwa Meneja wa Mradi kuhakikisha malipo kwa wafanyakazi wote wanaoshiriki katika mradi huo, ikiwemo wakandarasi wa ndani, mafundi na vibarua, yanafanyika kwa wakati.

“Meneja wa Mradi simamia na hakikisha mafundi na vibarua wanalipwa kwa wakati fedha zinapotoka. Tunapokamilisha mradi wale wote waliohusika kufanya kazi walipwe malipo yao mara moja,” alisisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here