Maumivu nishati ya mafuta:Rais Trump aagiza jeshi kuzingira lango la Strait of Hormuz,hakuna meli kupita

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuanza mara moja kwa operesheni ya kijeshi ya kuzingira lango la Bahari la Hormuz kufuatia kushindwa kwa mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Iran yaliyofanyika nchini Pakistan.
Picha na Mtandao.

Hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo ya saa zaidi ya 20 yaliyofanyika mjini Islamabad kuvunjika bila kufikiwa kwa makubaliano, huku pande zote zikishindwa kukubaliana juu ya suala nyeti la mpango wa nyuklia wa Iran.

Kwa mujibu wa taarifa ya Rais Trump leo Aprili 12,2026, Jeshi la Wanamaji la Marekani limeagizwa kuzuia meli zote zinazoingia au kutoka katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti njia hiyo muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta.

Mazungumzo hayo, yaliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Marekani,JD Vance yalivunjika baada ya Iran kukataa kutoa dhamana ya kusitisha kabisa mpango wake wa silaha za nyuklia, jambo ambalo Marekani ilisisitiza kuwa ni sharti kuu la makubaliano.

Kwa upande wake, Iran imeeleza kuwa madai ya Marekani yalikuwa makubwa kupita kiasi na hayakuzingatia misingi ya kuaminiana kati ya mataifa hayo mawili.

Rais Trump amesisitiza kuwa, meli yoyote itakayojaribu kupita katika mlango huo itazuiwa au kukamatwa, na kuongeza kuwa vikosi vya Marekani vitaondoa mabomu ya majini yanayodaiwa kuwekwa na Iran katika eneo hilo.

Aidha, ameonya kuwa hatua yoyote ya uchokozi kutoka Iran itajibiwa kwa nguvu kubwa zaidi ya kijeshi, huku pia akitishia kushambulia miundombinu muhimu ya Iran iwapo haitasitisha mpango wake wa nyuklia.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwa na athari kubwa kiuchumi duniani, hasa katika soko la mafuta, kwa kuwa Bahari ya Hormuz ni njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta ya dunia.

Aidha, nchi kadhaa zinazoagiza mafuta kutoka Iran, ikiwemo China na India, zinaweza kuathirika na mabadiliko hayo, hali inayoweza kuongeza mvutano wa kidiplomasia kati ya Marekani na mataifa hayo.

Wakati huo huo, Iran imeonya kuwa hatua ya kuizingira njia hiyo itachukuliwa kama uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na imeahidi kujibu ipasavyo iwapo itachokozwa.

Mvutano huo unakuja katika kipindi ambacho vita kati ya pande hizo bado vinaendelea kwa kiwango fulani, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano yaliyolenga kutoa nafasi kwa mazungumzo ya amani.

Kuanzishwa kwa mzingiro huo kunazidisha hatari ya kuongezeka kwa mgogoro wa kijeshi katika Mashariki ya Kati, huku juhudi za kidiplomasia zikionekana kudhoofika.

Aidha,hatua hiyo pia inaibua hofu ya kuyumba kwa uchumi wa dunia endapo usafirishaji wa mafuta kupitia njia hiyo muhimu utaendelea kuvurugika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here