Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus afanya ziara ya kihistoria nchini,akutana na mwenyeji wake Dar

DAR-Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Belarus Mheshimiwa Maxim Ryzhenkov amefanya mazungumzo na Mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo jijini Dar es Salaam Aprili 28, 2026, yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kupanua ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja kati ya Tanzania na Belarus.
Mheshimiwa Maxim Ryzhenkov yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Aprili 28 hadi 30 2026 ambapo pia atakutana na Mawaziri mbalimbali wa kisekta kwa madhumuni ya kujadili masuala ya kuimarisha ushirikiano katika sekta zao.
Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Belarus ambapo walisisitiza azma ya kupunguza urasimu unaoweza kuathiri biashara na uwekezaji.

Kufanikisha dhamira hii, Mheshimiwa Waziri Kombo amependekeza Serikali ya Belarus kuanzisha Ubalozi kamili hapa nchini ili kusaidia kukuza diplomasia ya uchumi na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya pamoja.

Kuhusu Mageuzi ya Kilimo na Matumizi ya Mitambo, Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa hasa kwa kuzingatia uzoefu wa Belarus katika uzalishaji wa mitambo ya kilimo.
Viongozi hao wamehimiza uwekezaji katika uunganishaji wa matrekta, uzalishaji wa mbolea, na uhamishaji wa teknolojia za umwagiliaji ili kuongeza tija na thamani ya mazao.

Kuhusu ushirikiano katika Nishati na Miundombinu, Waziri Kombo ameialika Belarus kushiriki katika uwekezaji na huduma za kihandisi, hususan katika maendeleo ya mafuta na gesi, nishati jadidifu (jua, upepo na maji), pamoja na uimarishaji wa miundombinu ya gesi hapa nchini.
Pia, kuhusu Uwekezaji na Sekta ya Afya na Dawa, Mawaziri hao wamejadili namna ya kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi wa uagizaji.

Katika majadiliano hayo Kampuni ya BELPHARMPROM ilionesha nia ya kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD) katika uzalishaji na
usambazaji wa bidhaa za afya.

Katika eneo la elimu na kujengeana uwezo Mhe. Waziri Kombo ameishukuru Serikali ya Belarus kwa kuendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Tanzania, hususan katika fani ya tiba kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Viongozi hao pia, wamejadili kupanua ushirikiano katika fani za uhandisi, sayansi ya data na akili unde, na kuimarisha uhusiano kati ya taasisi za elimu ya juu, kikiwemo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo cha Karume Zanzibar na Chuo Kikuu cha Mzumbew.

Kuhusu Utalii na Biashara Mheshimiwa Waziri ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka Belarus wanaotembelea Tanzania, ambapo zaidi ya watalii 6,000 wametembelea Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

Katika biashara, Tanzania na Belarus zimejipanga kuboresha uwiano wa biashara kwa kukuza mauzo ya bidhaa za Tanzania kama kahawa, parachichi na maua katika soko la Belarus.
Mheshimiwa Waziri Kombo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemshukuru Mheshimiwa Waziri Ryzhenkov kwa ziara yake na kwa dhamira yake ya kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Belarus.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here