DAR-Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza rasmi Baraza Kivuli jipya la Mawaziri kwa kipindi kinachofuata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kikisema kitaendelea kuisimamia Serikali kwa nguvu zaidi ndani na nje ya Bunge ili kuhakikisha uwajibikaji na ulinzi wa maslahi ya wananchi vinaendelea kupewa kipaumbele.
Akizungumza leo Mei 18, 2026, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Jonas Semu, alisema matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 yameendelea kutoa uwakilishi mwembamba wa vyama vya upinzani Bungeni, hali ambayo imelazimu vyama vya siasa kutafuta mifumo mbadala ya kuisimamia Serikali na kuendeleza siasa za hoja nje ya mhimili wa Bunge.
Semu amesema, baraza hilo linaendelea kutekeleza azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa la mwaka 2022 lililoanzisha mfumo rasmi wa Baraza Kivuli ndani ya chama hicho kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata sauti mbadala yenye nguvu katika masuala ya kisera, uwajibikaji na usimamizi wa Serikali.
Kwa mujibu wa Semu, hili ni Baraza la tatu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, ambapo kwa kipindi cha miaka minne iliyopita limekuwa jukwaa muhimu la kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi pamoja na kushawishi mjadala wa kitaifa kuhusu masuala muhimu ya maendeleo, uchumi na utawala.
Amesema, tofauti na Baraza zilizopita, Baraza jipya litahusisha wabunge waliopo Bungeni sambamba na wataalamu pamoja na wanachama wenye uzoefu waliopo nje ya Bunge, hatua inayolenga kuongeza ubora wa uchambuzi wa sera na kupanua wigo wa usimamizi wa Serikali.
Katika muundo huo mpya, Semu amesema chama kimezingatia uwiano wa kijinsia ambapo wanawake 11 kati ya wasemaji 23 walioteuliwa ni wanawake, sawa na asilimia 47 ya wajumbe wote wa Baraza hilo.
Katika uteuzi huo, Isihaka Rashid Mchinjita ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu Kivuli huku Luhaga Joelson Mpina akiteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu Kivuli pamoja na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini. Nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi imechukuliwa na Idrisa Abdul Kweweta.
Wengine walioteuliwa ni pamoja na Nagy Kaboyoka ambaye atakuwa Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu pamoja na Mnadhimu wa Baraza, Ado Shaibu Ado katika Ofisi ya Rais – Mipango, Fedha na Hifadhi ya Jamii, pamoja na Pavu Abdallah Juma katika Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora.
Majina mengine yaliyotajwa katika Baraza hilo ni pamoja na Kulthum Jumanne Mchuchuli, Said Ali Mbarouk, Rashid Habib Ali, Peter Madeleka, Fatma A. Fereji, Dkt. Elizabeth Sanga na Riziki Shahari Ngwali ambao watakuwa wasemaji wa sekta mbalimbali.
Akizungumzia mwelekeo wa Baraza hilo kwa mwaka huu, Semu amesema wajumbe wote wanapaswa kuongeza nguvu katika kusimamia uwajibikaji ndani ya Serikali na taasisi zake, akisisitiza kuwa taifa haliwezi kujengwa katika mazingira ya matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa rasilimali za umma pamoja na kutowajibika kwa viongozi.
Katika hotuba yake, Semu ameikosoa Serikali kwa kile alichodai kuwa ni kuendelea kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na ukosefu wa uwajibikaji.
Amesema kupitia uchambuzi wa ripoti za Office of the Controller and Auditor General (CAG), chama hicho kimebaini zaidi ya shilingi trilioni saba zimepotea au kutumika bila maelezo ya kuridhisha.
Aidha, alisema taifa limeendelea kushuhudia matukio ya mauaji, uporaji wa ardhi za wananchi pamoja na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za umma huku hatua za uwajibikaji zikidaiwa kutokuwa za kuridhisha.
Kutokana na hali hiyo, Semu aliwataka wajumbe wa Baraza hilo kuwa mstari wa mbele katika kulinda haki za wananchi, kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma na kuhakikisha hakuna kiongozi anayekuwa juu ya sheria.
“ACT Wazalendo itaendelea kuwa sauti ya wananchi waliokata tamaa ya kusikilizwa, na Baraza hili litakuwa mstari wa mbele kuhakikisha hakuna anayekuwa juu ya sheria wala anayefanya matumizi mabaya ya mamlaka bila kuhojiwa,” alisema Semu.
