BoT na HESLB kuimarisha elimu ya fedha kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini

DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua rasmi utekelezaji wa hati ya makubaliano yenye lengo la kuimarisha elimu ya fedha kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika tarehe 18 Mei 2026 katika ofisi za BoT jijini Dodoma, Gavana wa BoT, Bw.Emmanuel Tutuba, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuwawezesha vijana wa Kitanzania kwa kuwapatia maarifa ya kifedha na stadi muhimu za usimamizi wa fedha.

Alieleza kuwa kupitia ushirikiano huo, wanafunzi watanufaika na programu maalum ya elimu ya fedha itakayopatikana kupitia mfumo wa akaunti binafsi ya mwanafunzi unaojulikana kama Students’ Individual Permanent Account (SIPA).

Mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa elimu ya fedha kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kote nchini kupitia majukwaa ya kidijitali.
Gavana Tutuba alibainisha kuwa programu hiyo itajikita katika maeneo muhimu ikiwemo uandaaji wa bajeti, uwekaji wa akiba, matumizi sahihi ya mikopo, mipango ya kifedha, matumizi ya huduma za kifedha kidijitali, pamoja na ulinzi wa mtumiaji wa huduma za fedha.
Aliongeza kuwa maarifa hayo yatawasaidia wanafunzi na wahitimu kuwa na nidhamu ya kifedha, kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, na hatimaye kuchangia kwa ufanisi katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alieleza kuwa taasisi hiyo inatambua wajibu wake mkubwa katika kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano hayo unakuwa wenye tija na mafanikio.
Aidha, alibainisha kuwa HESLB itashirikiana na BoT katika kupitia, kuboresha na kupakia maudhui hayo ili kuhakikisha yanakuwa sahihi, bora na yenye manufaa kwa wanafunzi. 

Pia, taasisi hiyo itaweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na tathmini utakaosaidia kupima ufanisi wa programu hiyo na kufanya maboresho pale inapobidi.
Uzinduzi huo unaashiria hatua muhimu katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuwajengea vijana msingi imara wa ustawi wa kifedha, sambamba na kukuza uchumi endelevu wa Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here