Air Tanzania kuanza safari za Dar es Salaam hadi Moscow nchini Urusi

NA DIRAMAKINI

SHIRIKA la Ndege Tanzania (Air Tanzania) limepanga kuanzisha safari mpya za ndege kati ya Dar es Salaam na Moscow kupitia Seychelles, katika hatua inayotarajiwa kuwa safari yake ya kwanza kuelekea Bara la Ulaya kwa mtandao wake wa kimataifa wa usafiri wa anga.
Mpango huo unakuja baada ya shirika hilo kuanza safari zake kwenda Seychelles, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kurahisisha muunganiko wa safari hiyo mpya kuelekea Urusi.

Endapo mpango huo utakamilika, safari hiyo itaongeza wigo wa huduma za usafiri wa anga kati ya Tanzania na mataifa ya Ulaya Mashariki pamoja na kuimarisha fursa za biashara,utalii na usafiri wa kimataifa.

Kwa sasa, Air Tanzania bado linakabiliwa na vikwazo vya matumizi ya anga katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), hali inayolizuia shirika kuendesha safari katika baadhi ya maeneo ya bara hilo chini ya mifumo ya udhibiti wa usalama wa anga ya umoja huo.

Hata hivyo, kuanzishwa kwa safari za kwenda Urusi kunatajwa kuwa nje ya mfumo wa kanuni za Umoja wa Ulaya, jambo linaloweza kulipa shirika hilo nafasi ya kupanua huduma zake za kimataifa bila kuathiriwa moja kwa moja na masharti hayo ya EU.

Wachambuzi wa sekta ya usafiri wa anga wanaeleza kuwa,hatua hiyo inaweza kuongeza ushindani wa Air Tanzania katika soko la kimataifa huku ikiimarisha nafasi ya Dar es Salaam kama kitovu muhimu cha usafiri wa anga katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, safari hizo zinatarajiwa kuchochea mahusiano ya kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania, Seychelles na Urusi kupitia ongezeko la safari za abiria na mizigo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here