NJOMBE-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshiriki kikamilifu Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Lunyanywi mkoani Njombe, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika tukio hilo, mshindi wa Tuzo ya Mfanyakazi Bora wa Benki Kuu, Bw. Rweyemamu Barongo, alipokea hati ya kutambua mchango wake iliyotolewa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA). Hati hiyo inaakisi juhudi na weledi wa watumishi wa Benki Kuu katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Sambamba na maadhimisho ya kitaifa, Benki Kuu ya Tanzania ilishiriki pia katika maadhimisho yaliyofanyika katika kanda mbalimbali nchini kupitia ofisi zake zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Mwanza na Mtwara, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuenzi mchango wa wafanyakazi kote nchini.










