NA DIRAMAKINI
BODI ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara (TPLB) imethibitisha rasmi kuwa mchezo wa dabi ya Kariakoo kati ya Simba SC na Yanga SC utakaopigwa Mei 3, 2026, utaongozwa na jopo la waamuzi kutoka nchini Morocco.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 2, 2026 imeeleza kuwa, mwamuzi wa kati wa pambano hilo atakuwa Hamza El Fareq, ambaye anatarajiwa kuongoza mchezo huo utakaochezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuanzia saa 12:00 jioni.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Hamza El Fareq atasaidiwa na waamuzi wasaidizi wawili kutoka taifa hilo hilo, ambapo Lahsene Agaou atakuwa mwamuzi msaidizi namba moja, huku Hamza Massiri akiteuliwa kuwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Nafasi ya mwamuzi wa nne itashikiliwa na Mustapha Kechaf.
Uteuzi wa waamuzi wa kimataifa kwa mchezo huo unatafsiriwa kama juhudi za kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi wenye weledi, haki na uwazi katika moja ya michezo yenye ushindani mkubwa na mvuto wa kipekee katika soka la Tanzania.
Dabi ya Kariakoo kati ya Simba SC na Yanga SC imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa soka nchini na nje ya mipaka, ikihusisha ushindani wa kihistoria kati ya klabu hizo kongwe zenye mafanikio makubwa.
Mchezo wa mwaka huu unatarajiwa kuwa na ushindani mkali huku kila upande ukilenga kujihakikishia alama muhimu katika msimamo wa ligi.
