NA DIRAMAKINI
MKUTANO wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa ya BRICS umehitimishwa mjini New Delhi, India bila kutolewa kwa taarifa ya pamoja, hali iliyoonesha wazi kuwepo kwa tofauti kubwa za kisiasa miongoni mwa nchi wanachama kuhusu mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
Badala ya taarifa ya pamoja, India ambayo ni mwenyekiti wa BRICS mwaka 2026 ilitoa taarifa ya mwenyekiti pekee, ikikiri kwamba wanachama walikuwa na mitazamo tofauti kuhusu hali ya usalama katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati.
Kundi la BRICS linajumuisha nchi za Brazil, Urusi, India, China, Afrika Kusini, Ethiopia, Misri, Iran, Falme za Kiarabu (UAE) na Indonesia.
Tofauti kuu katika mkutano huo zilichangiwa na mvutano kati ya Iran na UAE, ambazo kwa sasa ziko katika pande tofauti kwenye vita vinavyoihusisha Iran dhidi ya Marekani na Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi aliishinikiza BRICS kulaani mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya taifa hilo, huku pia akiituhumu UAE kwa kushiriki katika operesheni za kijeshi dhidi ya Tehran.
Kwa upande wake, UAE ilipinga madai hayo na kulaani mashambulizi ya Iran dhidi ya maeneo yake.
Kutokana na mvutano huo, wanachama walishindwa kufikia mwafaka wa pamoja kuhusu tamko rasmi la mkutano huo.
India ilieleza kuwa,baadhi ya nchi wanachama zilitoa misimamo tofauti kuhusu umuhimu wa diplomasia, kuheshimu mamlaka ya mataifa, usalama wa njia za baharini na ulinzi wa raia katika maeneo ya migogoro.
Pamoja na tofauti hizo, mawaziri hao walikubaliana kuhusu umuhimu wa nchi za Kusini mwa Dunia kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi, kisiasa na kiusalama zinazoukabili ulimwengu kwa sasa.
Pia walisisitiza haja ya kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana na migogoro ya kimataifa.
Mkutano huo pia ulijadili athari za mgogoro wa Mashariki ya Kati kwa uchumi wa dunia, hususan usalama wa usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya biashara ya nishati duniani.
India ambayo ni moja ya waagizaji wakubwa wa mafuta duniani, imeeleza wasiwasi wake kuhusu usalama wa njia hiyo kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi katika eneo hilo.



